Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Saturday, January 14, 2012

Katibu NCCR ashushwa jukwaani kwa Kafulila


Ruhuza juzi alilazimika kushuka jukwaani baada ya kuzomewa na wananchi wakati akihutubia mkutano wa hadhara wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.

Ruhuza amepiga kambi mkoani Kigoma tangu Januari mosi mwaka huu, akiongoza kikosi maalumu cha viongozi wa chama hicho, kinachoendesha operesheni ya ufuatiliaji wa utekelezaji ahadi za wabunge na madiwani wake.

Rwehuza alikumbana na balaa hilo pale alipojaribu kuwaeleza wananchi hao juu ya uamuzi wa Halmashauri Kuu ya NCCR- Mageuzi, kumvua uanachama kada wa chama hicho ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila.

Operesheni ya viongozi hao mkoani Kigoma, ilianza siku siku chache baada Kafulila kuanza ziara mkaoni humo, kwa kile alichoeleza, kutembelea wapigakura wake, ambapo pamoja na mambo mengine, amekuwa akielezea hatma ya ubunge wake baada ya kuvuliwa uanachama Desemba 17 mwaka jana.

Hotuba ya Ruhuza
Akiwa jukwaani, katika hotuba yake Ruhuza alianza kuzungumzia mambo mbalimbali ya chama hicho pamoja na migogoro ya ardhi katika Mkoa wa Kigoma na kuwataka wananchi wa Kasulu kupigania ardhi yao aliyodai inapokwa na Serikali, kwa kisingizio cha kufanywa hifadhi ya taifa.

Ruhuza alisema ni kweli sheria inakataza wananchi kwenda kwenye maeneo ya hifadhi, lakini wananchi hawajui mipaka ya maeneo ya hifadhi na kuwa hilo ni kosa la Serikali kutoweka alama zozote kuonyesha mipaka ya maeneo hayo.

“Suala hili, napenda niwaelekeze kitu kimoja ndugu zangu wananchi wa Kasulu. Ardhi ni suala nyeti sana katika nchi hii na suala nyeti katika dunia, ukikosa umiliki wa ardhi hata kabila na ukoo wako unafutika,” alisema Ruhuza.

Alisema wananchi waione ardhi kama urithi waliopewa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na  waipiganie kwa nguvu zote na kuwaagiza wabunge na madiwani kupambana na tatizo hilo, ili ardhi imilikiwe na wananchi wa Kasulu.

Pamoja na wananchi kumsikiliza kwa makini, upepo uligeuka ghafla pale Ruhuza alipozungumzia suala lililokuwa likisubiriwa kwa hamu, la kuvuliwa uanachama Mbunge Kafulila.

Ruhuza alitetea uamuzi wa chama hicho kumfukuza uanachama Kafulila kwa maelezo kwamba alikiuka taratibu na miongozo ya chama kwa kutotii sheria na Katiba ya chama hicho, jambo lililosababisha NEC ya NCCR- Mageuzi, kumvua uanachama na kumpa wiki mbili za kukata rufaa kwenye Mkutano Mkuu wa Chama hicho.

Wakati akiendelea kutoa maelezo hayo, umati uliokuwa umekusanyika kwenye mkutano huo, ulilipuka na kuanza kumzomea huku baadhi walisikika wakisema:

“Hatukutaki..., ondoka..., teremka huna jipya! Chama kimekufa, tunamtaka Kafulila!”

Ingawa Ruhuza alijitahidi kuwatuliza wananchi hao kwa kutumia Kiha ambayo ni lugha ya wakazi wengi wa mkoa huo, bado aliendelea kuzomewa, hatua iliyosababisha  Mbunge wa Kasulu Vijijini, Zaituni Buyogera  apande jukwaani na kudai wanafunga mkutano huo kutokana na kelele za wananchi hao, waliokataa kuwasikiliza viongozi hao.

Pamoja na tafrani hiyo, Ruhuza alijitahidi kuendelea na hotuba yake lakini sauti yake ilizidiwa na kelele za wananchi hao walioendelea kumzomea, wakisisitiza kuwa wanamtaka Kafulila.

Kabla ya Mbunge Buyogera kumtoa Ruhuza jukwaani, wananchi hao pia walianza kumzomea ingawa awali walimsikiliza kwa umakini.

Kabla ya Ruhuza kuzomewa Kasulu, imedaiwa kuwa zimekuwepo zomeazomea kwenye mikutano mingine kadhaa iliyofanyika Kata ya Nguruka ambapo Mwenyekiti wa Makamishna wa NCCR -Mageuzi, Peterson Mshenyela, alikumbwa na balaa hilo.Kila wakati Mshenyela alipomsema vibaya Kafulila , wananchi walimzomea," alisema mtoa habari yetu.

Ruhuza asimulia kilichotokea
Alipoulizwa jana, Ruhuza alikiri kuibuka kwa mtafaruku kwenye mkutano huo na kueleza  kwamba, kulikuwa na watu waliotaka azungumzie suala la Kafulila, lakini wengine walikuwa hawataki lizungumzwe na kuzua malumbano hayo.

Ruhuza alileza kuwa watu waliofanya fujo hizo hawazidi 10."Walikuwa wanapiga kelele, lakini baadaye watu hao walikiri kwamba walitumwa kufanya fujo hizo."

Kafulila alivuliwa uanachama baada ya kura 38 zilizopigwa kati ya 64 kwenye kikao cha NEC ya chama hicho, kutaka ang'oke kwa tuhuma za kuzungumza mambo ya chama nje ya vikao na kutaka kumpindua Mbatia.

Hata hivyo, hatma ya ubunge wake kwa sasa iko mikononi mwa Mahakama ambayo tayari imetoa zuio la utekelezaji wa uamuzi huo wa Desemba 17 huku mbunge huyo pia, akiwa amefungua kesi ya msingi. 


No comments: