Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Friday, January 13, 2012

Kabwe Zitto na mkakati wa kupambana na mfumuko wa bei

OFISI ya Taifa ya Takwimu inaonesha kwamba, wakati mfumuko wa bei mwezi Julai mwaka huu katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2011/2012 ilipokuwa inaanza ulikuwa asilimia 13,
lakini hadi kufikia Novemba mwaka jana ulifikia asilimia 19.2.

Katika tafsiri ya kiuchumi hiyo inamaanisha kuwa , Bajeti ya Serikali iliyopitishwa na Bunge mwezi Juni 2011, imepunguza uwezo wa kununua bidhaa na huduma kwa takribani asilimia 6.


Kwa mujibu wa taarifa ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, hiyo ni sawa na Sh bilioni 780 kuyeyuka katika bajeti katika kipindi cha miezi minne tu ya utekelezaji wa wake.


Zitto anafafanua kuwa kutokana na kasi ya ukuaji wa mfumuko wa bei ni dhahiri kwamba, itakapofika mwisho wa mwaka wa Bajeti Serikali itakuwa imepoteza kwa kiasi kikubwa uwezo

wa kununua bidhaa na huduma kwa zaidi ya robo ya bajeti yake.

Anasema kuwa mbaya zaidi kwa wananchi kwani mfumuko wa bei za vyakula umekua kwa kasi kikubwa mno. Ofisi ya Takwimu imeonesha kuwa wakati mfumuko wa bei za vyakula ulikuwa asilimia 14.8 mwezi Julai, umefikia asilimia 24.7 mwezi Novemba 2011.


Anasema ukilinganisha na bei za vyakula mwaka 2010, mwananchi amepoteza uwezo wa kununua chakula kwa zaidi ya robo katika ya Novemba 2010 na Novemba 2011. Jumla ya

vyakula ambavyo mwananchi alinunua kwa Sh 10,000 mwaka 2010, sasa atanunua kiwango kile kile kwa Sh 12,500.

Katika taarifa yake anafafanua kuwa bei za vyakula zimeongezeka kwa kiwango hiki ilhali kipato cha mwananchi aghalabu kipo pale pale. Anasema mwathirika mkubwa ni mwananchi wa kawaida wa kijijini ambaye mapato yake ni kidogo na hivyo sehemu kubwa huyatumia kununua chakula.


Anasema ukiangalia kwa undani utakuta mfumuko wa bei wa bidhaa kama mchele, sukari, nyama na samaki umekua maradufu. Bei ya mchele imekua kwa asilimia 50, sukari asilimia

50, nyama asilimia 30 na Samaki kwa takribani asilimia 40.

Bidhaa hizi zote ni muhimu sana kwa afya ya binadamu na hasa watoto kwa upande wa vyakula

vya protini. “Tusipokuwa makini na kupata majibu sahihi ya tatizo la mfumuko wa bei za vyakula, wananchi wengi na hasa watoto watapata utapiamlo na Taifa kuingia gharama kubwa katika kuwapatia huduma ya afya,”anaeleza Zitto.

Kwa upande wa bidhaa zisizo za vyakula, anasema mfumuko wa bei wa mafuta ya taa na gesi asilia unapaa kwa kasi kama moto wa nyikani. Wakati mafuta ya taa yamepanda bei kwa asilimia 71 katika ya mwezi Novemba mwaka 2010 na mwezi Novemba 2011, bei ya gesi asilia imepanda kwa asilimia 35.


Anasema madhara ya hali hii ni makubwa mno maana wananchi watakimbilia kwenye matumizi ya mkaa na kuni, hata hivyo bei za mkaa zenyewe zimepanda kwa asilimia 24.


“ Kwa hali hii, na kutokana na ukweli kwamba wananchi wengi wa Tanzania wapo kwenye mpaka wa umasikini na daraja la kati chini, juhudi za muongo mzima za kupunguza

umasikini zitafutwa ndani ya mwaka mmoja tu,”anasema Zitto.

Anasema mfumuko wa bei unasukuma Watanzania wengi zaidi kwenye dimbwi la umasikini, unapunguza uwezo wa Serikali kutoa huduma za jamii kupitia bajeti na hata kutimiza mipango ya miradi ya maendeleo kama miundombinu ya barabara, umeme, bomba la gesi na madaraja nk.


Akizungumzia mikakati ya kupamba na hali hiyo, anasema, hatua madhubuti zinapaswa kuchukuliwa ili kuuhami uchumi na kupunguza upandaji wa kasi wa gharama za maisha.

Anasema kuwa hatua hizo ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa chakula kwa kuweka mbinu za kukuza uchumi wa vijijini ni njia mojawapo endelevu ya kupunguza mfumuko wa bei hapa nchini.

Anasema Serikali iruhusu na ivutie kwa kasi na kutoa vivutio kwa wazalishaji binafsi wa sukari na mpunga katika mabonde makubwa. Anasema vyakula vilivyolundikana mikoa ya Mbeya, Iringa na Rukwa ambapo Serikali iliahidi kununua na kutotimiza ahadi yake vinunuliwe mara moja na kusambazwa mikoa yenye shida ya chakula kama Mwanza, Mara, Kagera na mikoa ya Kaskazini.


Anasema wakati huu ambapo tunaweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wa chakula, Serikali inunue chakula cha kutosha na hasa mchele na sukari kutoka nje na kukisambaza kwenye soko ili kupunguza upungufu wa bidhaa katika masoko.


Anaeleza kuwa mfumo uliotumika kununua sukari tani laki moja hivi karibuni usitumike tena kwani ulizaa rushwa ya hatari na ufisadi ambao haujaripotiwa kwenye kutoa vibali. Anasema kuwa mkakati mwingine Wizara ya Kilimo iruhusu wauzaji kutoka nje walete sukari nchini moja kwa moja na kununuliwa na Bodi ya Sukari kisha kuiuza kwa wauzaji wa jumla.


Anasema mfumo wa kutoa vibali umeonesha kutokuwa na tija na kwa kweli kunufaisha maofisa wachache wa Wizara ya Kilimo na Bodi ya Sukari. Kwa upande mwingine nasema kuwa ushuru wote unaokusanywa kwenye mafuta ya taa upelekwe Wakala wa Nishati Vijijini ili

kufidia kupanda kwa bei ya mafuta ya taa.

No comments: