Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Tuesday, January 3, 2012

NCCR kumfukuza Kafulila si kukijenga chama

HALMASHAURI Kuu ya NCCR-Mageuzi, katika kikao chake cha Desemba 17, mwaka huu, ilimvua uanachama Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, wakimtuhumu kuvujisha siri za vikao.

Uamuzi huo wa Halmashauri ya chama hicho uliotangazwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Samwel Ruhuza, umethibitisha kuwa kikao hicho ni cha juu katika uamuzi, lakini hakijafunga milango kuwapa nafasi wanachama wake waliofukuzwa kukata rufaa.

Katika kumba kumba hiyo ya kuwafukuza wanachama, walikuwamo wenzake watatu na wengine 19 walipewa karipio kali, kitendo ambacho wanasiasa wengi wamenyooshea vidole kuwa hakijazingatia demokrasia, siasa na nafasi ya wananchi wa jimbo la Kigoma Kusini.

Kafulila na Hashim Rungwe aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, wamevuliwa uanachama pamoja na aliyekuwa Kamishna wa chama hicho Mkoa wa Tanga, Mbwana Hassan na mwanachama mwingine Yothamu Lubungira, lakini Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali, pamoja na wenzake 19 walinusurika kuvuliwa uanachama lakini wakapewa karipio kali.

Katika kujinasua na kitanzi cha Halmashauri Kuu ya chama hicho, Kafulila, Rungwe, Mbwana Hassan na Lubungira, wamezungumza na wazee wa chama hicho ili kuona uwezekano wa kupewa msamaha au kuwaombea radhi kwenye uongozi wa juu wa chama.

Kwenye kikao cha Halmashauri Kuu, pia walijadili na kupokea utetezi wa Mwenyekiti Taifa wa chama hicho, James Mbatia, kutokana na tuhuma zilizowasilishwa na Mbwana pamoja na wanachama wengine 26, waliosaini hati ya kutokuwa na imani naye.

Ruhuza anasema pamoja na tuhuma hizo, wajumbe hao wa NEC walimuona Mbatia hana tuhuma za kujibu na kuzitupilia mbali na kutoa maazimio matatu.

Badala yake, Halmashauri Kuu ilimpa pole na pongezi Mwenyekiti wa Taifa kwa kuzushiwa tuhuma zisizo na msingi na kuahidi kuwa chama hakitavumilia, kuona wanachama au viongozi wanakuwa watovu wa nidhamu na wanaleta migogoro yenye mwelekeo wa kukibomoa au kukidhoofisha chama.

“Hivyo Halmashauri Kuu ilimuona Mbatia kuwa kiongozi safi, hodari na shujaa wa chama” anasema Ruhuza. Mwanasheria wa NCCR Mageuzi, Dk. Sengondo Mvungi, anasema Kafulila hawezi kukata rufaa sehemu yoyote dhidi ya uamuzi wa kumfukuza uanachama, kwa mujibu wa kanuni ya 7 (2) ya chama hicho, lakini mwanachama ana haki ya kujitetea mbele ya kikao cha chama kinachohusika katika mashitaka au madai yoyote, na kuwa na haki ya kukata rufaa kwenye vikao vya juu iwapo mhusika hakuridhika na uamuzi wa kikao cha chini.’’

Halmashauri ya chama hicho iliwapa siku 14 za kukata rufaa Kafulila na wanachama wengine watatu kwenye mkutano mkuu wa chama hicho, kupinga uamuzi huo dhidi yao. Uamuzi huo wa kumvua uanachama Kafulila na wenzake, umenyooshewa kidole na wanasiasa wengi akiwamo Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa.

Tendwa ambaye ni mlezi wa vyama vya siasa nchini, amemkingia kifua Kafulila na kuvitaka vyama vya siasa kutumia busara katika kutatua migogoro yake na siyo kutoa uamuzi wa kukomoana na kufukuzana uanachama.

Tendwa anasema migongano mingi, inatokana na udhahifu katika kuainisha ukomo wa madaraka na kwamba busara inatakiwa itumike, kutambua yale kiongozi anavyotakiwa kuamua na yale ambayo lazima apate ushauri kabla ya kutoa uamuzi wake.

Katika kujinasua na kuvuliwa uanachama, Kafulila alifanya kikao na baadhi ya wazee wa NCCR-Mageuzi, katika ofisi za chama hicho ili kuomba msaada kwao.

Mbunge wa Kasulu Vijijini (NCCR-Mageuzi), Zaituni Buyogera, anasema mara baada ya Kafulila kuhamia NCCR-Mageuzi, alikabidhiwa kutembea naye vijiji vyote vya Jimbo la Kigoma Kusini ili kumtambulisha kwa wanachama na wananchi.

Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali, anasema hatua ya kutopatikana ufanisi katika idara za umma, vikiwamo vyama vya siasa ni kukosekana nidhamu kwa kushindwa kufuata kanuni, taratibu na sheria kama ilivyotokea kwa mbunge wenzake.

Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, anasema uamuzi wa NEC dhidi ya Kafulila, utakubaliwa na Bunge iwapo demokrasia katika kufikia uamuzi huo ilizingatiwa. Wakati hayo yakiendelea, Chadema kimemkaribisha mbunge huyo kujiunga na chama hicho baada ya kufukuzwa NCCR-Mageuzi.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe, kupitia ukurasa wake wa Facebook anasema: “Kafulila akumbuke kwamba hakufukuzwa Chadema ila alijiondoa mwenyewe”. "Milango yetu ipo wazi kwa mujibu wa Katiba, Kanuni na taratibu za chama chetu," anasema Zitto.

Nape Nnauye anasema vijana kwenye vyama vya siasa, wanatakiwa washauriwe na kupewa maonyo badala ya kufukuzwa. Nape alivitaka vyama vya siasa, vijenge utamaduni wa kuvumiliana na kuwalea vijana kwa kuwafundisha, badala ya kuwafukuza uanachama, kitendo ambacho anakiona kuwa kinazidi kudidimiza demokrasia na siasa na hivyo kutoandaa viongozi wa kesho.

Pamoja uongozi wa NCCR-Mageuzi kutoa uamuzi wa kuwafukuza wanachama wake na wengine kuwapa karipio, kinatakiwa kufikiria mstakabali wa chama, wananchi wa Kigoma Kusini na mchango wa vijana katika nchi.

No comments: