Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Tuesday, December 27, 2011

Kafulila bado ni Mbunge wa Kigoma kusini

MAHAKAMA Kuu imetoa amri kusitisha kutekelezwa kwa uamuzi wa Halmashauri Kuu ya
Chama cha NCCRMageuzi wa kumfukuza uanachama Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila
hadi kesi aliyofungua itakapomalizika.

Uamuzi huo ulitolewa jana katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na Jaji Alise Chingwile kutokana na maombi ya zuio yaliyowasilishwa na Kafulila kupitia Kampuni ya Uwakili ya Asyla ya Dar es Salaam.

Wakili wa Kafulila kutoka kampuni hiyo, Daniel Welwel alisema maombi hayo waliyawasilisha Ijumaa iliyopita chini ya hati ya dharura, kupinga kuvuliwa uanachama.

Kwa mujibu wa Wakili huyo, katika maombi hayo, walidai kwamba uamuzi huo wa NCCR-Mageuzi ukitekelezwa dhidi ya Kafulila atakuwa amekosa sifa za ubunge na jimbo litakosa mbunge.

“Tukasema na kesi ya msingi itakuwa haina maana,” alidai Wakili wa mwanasiasa huyo kijana
aliyewahi pia kuwa mwanachama na kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Katika kesi ya msingi ambayo itatajwa Februari 21, mwakani, Kafulila kupitia kwa mawakili wake, anadai uamuzi wa NCCR Mageuzi haukuwa halali kwa sababu Katiba ya chama hicho haikufuatwa.

Vile vile anadai hakupewa haki ya kusikilizwa licha ya kwamba ni haki yake ya msingi.

Anadai pia kwamba wajumbe walioshiriki kupitisha uamuzi huo, wengine hawakuwa wajumbe halali.

Watu wanaomuunga mkono pamoja na walio karibu na mbunge huyo, akiwemo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), wameelezea kufurahishwa na uamuzi huo wa Mahakama.

“Kafulila kuendelea na ubunge..... Mahakama Kuu imetoa amri muda mfupi uliopita.

Ataendelea kuwa Mbunge mpaka hapo kesi ya msingi itakapokwisha. Mungu yupo pamoja na wanyonge siku zote,” alisema Zitto kupitia mtandao wa kijamii.

Wengine wamekaririwa wakifurahia kwa kusema hiyo ni habari njema kwa walalahoi kwa kuwa
Uchaguzi Mdogo ukifanyika ni maumivu kutokana na Bajeti ya Serikali kuhamishiwa kwenye
shughuli hiyo.

Uamuzi wa kumfukuza uanachama mbunge huyo pamoja na watu wengine sita akiwemo
Hashim Rungwe aliyegombea urais katika Uchaguzi Mkuu uliopita, ulifanyika Desemba 17, mwaka huu katika kikao cha NEC Taifa ya NCCR-Mageuzi jijini Dar es Salaam.

Chama hicho chenye wabunge wanne wote kutoka majimbo ya Mkoa wa Kigoma, kilitoa siku 14 kwa Kafulila na wenzake kukata rufani.

Naibu Spika Job Ndugai akizungumza na gazeti hili juu ya zuio hilo la Mahakama Kuu, alisema
suala hilo linahitaji wanasheria waliobobea watafsiri sheria ikizingatiwa kwamba Ofisi ya Bunge ilishapokea barua ya NCCR-Mageuzi ya kumvua uanachama mbunge huyo.

“Hapo panahitaji wanasheria wasaidie kutafsiri. Kama tumepata barua ya chama, sisi hatuna cha kufanya isipokuwa kutii. Kama Mahakama imefanya hivyo (kuzuia), Kafulila apeleke nakala ya uamuzi, tujue sheria inasemaje,” alisema Ndugai.

Alisisitiza kwamba, “huwezi kuwa Mbunge kama chama chako kimekukana. Spika anakuwa hana chaguo. Tunahitaji wanasheria waliobobea kutafsiri sheria.”

Awali, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah alikiri kwamba ofisi imekwishapokea barua ya
NCCR Mageuzi ya kumvua ubunge Kafulila na kwamba inafanyiwa kazi, ingawa hakuna muda maalumu wa kutenda kazi hiyo.

No comments: