Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Tuesday, December 27, 2011

Hospitali ya Maweni Kigoma yapata msaada

HOSPITALI ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni imekabidhiwa pikipiki 12 na gari moja vyenye
thamani ya Sh milioni 275, ili kukabiliana na changamoto za utoaji huduma na hasa katika kupunguza vifo vya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa uongozi wa hospitali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya alisema pikipiki 12 zimetolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii huku Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ikitoa gari moja aina ya Toyota Land Cruiser Hard Top.


Machibya alisema vifaa hivyo vimetolewa katika kukabiliana na uhaba wa vitendea kazi ikiwa ni mkakati wa Serikali wa kuboresha utoaji huduma katika sekta ya afya ili kutimiza Malengo ya Maendeleo ya Milenia.


Katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika kwenye Hospitali ya Mkoa, Machibya alisema vifaa hivyo vinapaswa kutumika kwa malengo yaliyokudiwa hasa kupunguza vifo vya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano mkoani humo.


Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa, Dk. Valentino Bhangi alisema vifaa hivyo vitagawanywa kwa halmashauri tatu kati ya nne za mkoani Kigoma kwa kuzingatia mahitaji ya halmashauri na alizitaja kuwa ni Kigoma Vijijini, Kasulu na Kibondo.

No comments: