Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Sunday, December 4, 2011

Kigoma katika hofu ya ongezeko la Ukimwi

HALI si shwari mkoani Kigoma kutokana na takwimu kuonesha kuwa hali ya maambukizi mkoani huenda ikaongezeka maradufu kuliko sasa.

Akizungumza katika maadhimisho ya kilele cha Siku ya Ukimwi kimkoa zilizofanyika katika kijiji cha Kazuramimba Wilaya ya Kigoma Mkuu wa Mkoa Kigoma, Issa Machibya alisema kuwa takwimu zilizochukuliwa kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu zinaashiria kuongezeka kwa maambukizi.


Akielezea kuhusu hali hiyo Machibya alisema kuwa katika kipindi hicho watu 31,910 walijitokeza kupima VVU kwa hiari ambapo kati yao 1,271 sawa na asilimia nne ya watu hao waligundulika kuwa na maambukizi ambayo inazidi asilimia 1.7 ya sasa.


Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa ni dhahiri hali hiyo inaashiria kwamba utafiti mpya wa ukusanyaji takwimu utakapofanyika hali hiyo itaongezeka maradufu.


Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka viongozi wa dini kutumia nafasi zao katika nyumba zao za ibada kuwasihi waumini wao umuhimu wa kufuata maadili ya dini zao jambo ambalo litasaidia kuwafanya kuingia kwenye vitendo vya ngono zembe na kuzidisha maambukizi mapya.


Akitoa taarifa kwenye maadhimisho hayo, Mratibu wa Ukimwi Mkoa Kigoma, Zilpa Kisonzela alisema kuwa kumekuwa na changamoto kubwa katika kukabiliana na maambukizi ya Ukimwi sambamba na kuwahudumia waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi mkoani humo.


Hata hivyo ametoa mwito kwa Serikali kuwachukulia hatua viongozi wa mashirika yasiyo ya kiserikali ambao hutumia fedha za miradi zinazotolewa na wafadhili.

No comments: