Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Friday, December 2, 2011

Viongozi wa vijiji wachochea migogoro kuuza ardhi kiholela Kigoma

MIGOGORO mingi ya ardhi inayotokea vijijini kwa sasa, inachangiwa kwa kiasi kikubwa na
tabia ya baadhi ya viongozi wa vijiji kuuza maeneo ya ardhi kwa wawekezaji, bila kuzingatia utaratibu wa utoaji ardhi wanaopaswa kuufuata.

Mratibu Ardhi wa asasi ya Caritas iliyo chini ya Kanisa Katoliki Jimbo la Kigoma, John Mutondo alisema hayo wakati wa mafunzo ya sera ya ardhi na sheria ya ardhi ya mwaka 1999.

Mutondo alisema kuwa hali hiyo inatokana na kutofahamika kwa sheria na sera ya ardhi kwa viongozi na kamati za ardhi za kata.

Alisema sheria ya ardhi inakidhi haja na matakwa katika kusimamia masuala yote ya ardhi na kutoa mamlaka kwa uongozi wa vijiji kugawa ardhi kulingana na mwongozo huo lakini tatizo ni viongozi na wananchi kutofahamu sheria hizo.

Kwa mujibu wa Mutondo, sheria na utaratibu wa utoaji ardhi unabainisha kiasi na ukubwa wa ardhi ambao uongozi wa vijiji unaweza kugawa lakini hilo halifanyiki.

Alisema badala yake viongozi wa vijiji wamekuwa wakigawa ardhi kwa wawekezaji bila kupata
maelekezo kutoka kwa wataalamu wa ardhi wa wilaya na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri jambo ambalo huzua migongano baadaye.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kirando, Bahati Chemba alisema kuwa kufanyika kwa mafunzo hayo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza migogoro ya ardhi katika maeneo yao na hasa wakati huu ambao ardhi imekuwa na thamani kubwa katika maendeleo ya mwanadamu.

No comments: