Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Monday, November 7, 2011

Watakiwa kuwa macho na wahamiaji haramu

MBIO za Mwenge wa Uhuru za siku mbili mkoani Kigoma zimemalizika huku kiongozi wa mbio hizo, Mtumwa Rashid akiwahadharisha wananchi kuwa macho na wahamiaji haramu katika maeneo yao.

Akizungumza katika maeneo mbalimbali mkoani hapa, Rashid aliwataka wananchi wa Kigoma kutopoteza urithi wa amani walioachiwa na rasilimali walizonazo kwa hadaa ya kupatiwa fedha na misaada kutoka kwa wahamiaji haramu.

Alisema kuwa kuongezeka kwa vitendo vya matumizi ya silaha katika mikoa ya Kigoma na Kagera kunatokana na wimbi la wakimbizi ambao wengi wao badala ya kukaa kwenye kambi rasmi, wako mitaani na baadhi yao wanaendesha vitendo vya ujambazi.

Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge alitoa mwito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao na kuacha kusikiliza maneno ya wanasiasa wanaowachochea wasishiriki.

Akizungumzia ujumbe wa Mwenge wa mwaka huu unaosema ‘tumethubutu, tumeweza na tunasonga mbele’, aliendelea kuwataka Watanzania kutosikiliza maneno ya kubeza yanayotolewa na wanasiasa kwamba miaka 50 Tanzania imeendelea kurudi nyuma kiuchumi na kimaendeleo.

Alisema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa za kimaendeleo, hususan katika sekta ya elimu.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya alisema kuwa mkoa wake umepiga hatua kubwa za kimaendeleo katika miradi ya maendeleo na utoaji huduma kwa jamii.

No comments: