Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Monday, November 7, 2011

Wanajeshi DRC wavamia Kigoma

SERIKALI ya Tanzania inawashikilia askari 20 wa kikosi maalumu cha Jeshi la Ulinzi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kwa kuingia nchini na silaha za kivita bila kutoa taarifa.

Mkuu wa Kikosi cha 24 cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Emmanuel Mchelli alisema jana kuwa wanajeshi hao kutoka DRC waliingia nchini Jumamosi saa saba mchana na kutia nanga katika bandari ya Kigoma.

Kwa mujibu wa Mchelli, wanajeshi hao waliingia nchini kwa kutumia boti ndogo iendayo kasi ikiwa imefungwa zana mbalimbali za kivita ikiwemo mabomu ya kutungulia ndege na mizinga midogo yenye uwezo wa kupiga umbali mrefu kutoka ilipo boti hiyo kinyume cha sheria za kimataifa.

Hata hivyo, Mchelli alisema JWTZ ilifanikiwa kuwakamata wanajeshi hao ambao walikuwa katika kikosi kilichoongozwa na Luteni Kanali Mohamed Mustapha.

Mbali na kiongozi huyo, pia boti hiyo ilikuwa na maofisa wanane wa jeshi hilo, wapiganaji wengine 11 akiwemo mwanamke ambaye ni mlinzi maalumu wa kiongozi huyo na fundi mmoja wa boti ambaye si mwanajeshi.

Baada ya kuwakamata Mchelli alisema kuwa wanajeshi hao walipelekwa katika kambi moja ya JWTZ mkoani Kigoma ambayo hakutaka kuitaja na zana zao za kivita na boti waliyokuwa wakisafiria vimewekwa chini ya ulinzi wa jeshi hilo.

Walipohojiwa sababu ya kuingia nchini na silaha nzito za kijeshi bila kutoa taarifa kwa mamlaka za nchi na za kiusalama, Mchelli alisema wanajeshi hao wa DRC walisema wameingia nchini kwa nia ya kuwachukua waasi wa nchi hiyo ambao walikimbilia mkoani Kigoma.

Wanajeshi hao kwa mujibu wa Mchelli, walisema kuwa mwanzoni mwa wiki iliyopita kulitokea mapigano kati yao na waasi ambao walikuwa na boti tano na katika mapigano hayo boti mbili za waasi zilizamishwa na tatu kukimbia ikiwemo moja ambayo ilikimbilia mkoani Kigoma.

Mchelli alisema wiki hiyo JWTZ iliwakamata waasi tisa walioingia nchini kupitia mkoani Kigoma wakitokea Ukanda wa Mashariki mwa DRC ambako kulikuwa na mapigano.

Waasi hao kwa maelezo ya Mchelli walikuwa wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao kwa risasi na walipelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni kupatiwa matibabu.

Tayari uongozi wa mkoa huo ulishaitisha kikao cha dharura cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kujadili hali hiyo na kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha mipaka na kuanza mchakato wa kushughulika na vikundi hivyo.

Mbali na kuanza kushughulika na vikundi hivyo, Mchelli alisema tayari wameshatoa taarifa kwa Mkuu wa Majeshi kuhusu hali hiyo na kwa uongozi wa juu wa nchi na kwa sasa wanasubiri maelekezo ya nini cha kufanya baada ya kufanyika mawasiliano kati ya viongozi wa Tanzania na wa DRC.

Mchelli alisema pamoja na ukubwa wa mpaka wa Tanzania na DRC, JWTZ imejipanga kudhibiti uingiaji holela wa wanajeshi kutoka nje.

No comments: