Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Monday, November 7, 2011

Waasi tisa DRC mbaroni Kigoma

WATU tisa ambao wanaaminika kuwa ni waasi kutoka nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Kigoma kwa kuingia nchini isivyo halali baada ya kuvuka mpaka kufuatia mapigano baina yao na serikali ya nchi hiyo.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma, Freizer Kashai aliwaambia waandishi wa habari kwenye bandari ndogo ya Kibirizi mjini Kigoma muda mfupi baada ya waasi hao kuwasili bandarini hapo kufuatia kujisalimisha kwao katika kijiji cha Mtanga kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma na kuletwa mjini hapa chini ya ulinzi wa jeshi hilo.

Kamanda Kashai alisema watu hao walikutwa na silaha za kivita ambazo zinahatarisha usalama wa nchi na kwamba walikuwa na boksi moja la Anti Air Craft, Bomu 175mm Anti Tank, risasi 3 za SMG, Radio call moja na MMG yenye risasi moja.

Aliwataja waasi hao kuwa ni Kikanda Saidi (Meja) Masuku Omari, Shabani Kambi, Samweli Kabwe, Maftaha Zuberi, Kasikilo Uledi, Vea Bomba na Kiombela Omari ambaye alikuwa kapteni wa meli na kwamba kati ya watu hao sita wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao katika mapigano hayo.

Alisema kuwa katika hatua za awali waasi hao watafikishwa katika Hospitali ya Mkoa Maweni kwa matibabu na baada ya matibabu hayo watafikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria.

Akizungumza na gazeti hili mmoja wa waasi hao, Masuku Omari alisema kuwa waasi hao walio chini ya kiongozi wao aliyemtaja kwa cheo kuwa ni Rais wa kikundi hicho Oluba Undji wameamua kupambana na serikali ya Kongo kutokana na kutokuridhishwa na masuala mbalimbali yanayo endeshwa na serikali ya nchi hiyo kwa sasa.

Kwa upande wao maofisa wa Ubalozi mdogo wa Kongo hapa mkoani Kigoma hawakutaka kuelezea kuhusu tukio hilo hadi hapo watakapopata taarifa za kina kutoka nchini mwao.

No comments: