Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Tuesday, November 22, 2011

Wafanyakazi hospitali ya mkoa Maweni hawamuamini Mganga Mkuu

WAFANYAKAZI wa Hospitali ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni, wamepiga kura ya kutokuwa na imani na Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk. Valentino Bangi, hivyo kuitaka Serikali kumuondoa kiongozi huyo.

Msimamo huo wa wafanyakazi hao umefikiwa katika kikao cha Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Tawi la Hospitali hiyo kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita chini ya uenyekiti wa Mwenyekiti wao, Silas Randa na kuhudhuriwa na Katibu wa chama hicho Mkoa, Amani Msuya.


Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na wajumbe 96, kati yao 86 walipiga kura ya kutokuwa na imani na kumkataa mganga huyo mkuu wa mkoa sambamba na kutoa tuhuma mbalimbali dhidi yake na Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo ya Mkoa, Dk. Amri Mulamuzi na kuiomba Serikali kuwaondoa mkoani humo.


Miongoni mwa tuhuma kubwa dhidi ya viongozi hao ni pamoja na kutolipwa madai na stahili zao mbalimbali na sababu kubwa ni uongozi wa mkoa kushindwa kusimamia madai yao wakati mwingine wakidaiwa kutumia fedha zinazokuja kwa ajili ya kulipwa madai yao kwa shughuli nyingine.


Madai hayo ya stahili zao wanazodai watumishi hao ni fedha za likizo, rufaa kwa ajili ya matibabu kwenye hospitali za rufaa, malipo ya saa za ziada na baadhi ya madai binafsi ya watumishi ambayo ni stahili zao.


Kama tuhuma hizo ni mwanzo tu wa vuguvugu hilo, walidai uongozi huo wa hospitali ya mkoa umekuwa ukitoa lugha zisizofaa, za kuudhi na za matusi kwa watumishi, hivyo kuchangia kuwakatisha tamaa watumishi.


Baada ya mkutano huo, Mwenyekiti wa Tughe Tawi la Hospitali ya Mkoa, Silas Randa alisema watachukua malalamiko hayo na tuhuma dhidi ya viongozi hao na kuwapelekea wahusika, lakini pia wataziwasilisha kwa Katibu Tawala wa Mkoa ambaye ndiye msimamizi na mamlaka ya nidhamu kwa uongozi wa hospitali hiyo.


Akizungumza na waandishi wa habari juu ya tuhuma hizo, Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk. Bangi alisema ingawa hazijamfikia, lakini zote ni uongo na hazina ukweli wowote, akisema ni majungu ya watumishi hao.


Akieleza sababu ya kutolipwa kwa madai mbalimbali ya watumishi, Dk. Bangi alisema natokana na upungufu wa fedha Serikali na ndiyo maana hata wao wanaletewa fedha kidogo kwa ajili ya malipo mbalimbali.


Akitoa mfano wa hilo, alisema kwa mwaka huu wa fedha, ofisi yake imetengewa Sh milioni 12 kwa mwaka kwa ajili ya malipo ya nauli za likizo kwa watumishi ambayo ni sawa ni Sh milioni moja kwa mwezi, jambo ambalo haliwezi kutoshelezwa mahitaji hata nusu ya watumishi 120 wa mkoa huo.


Kuhusu lugha za kuudhi na matusi, alisema hiyo inatokana na baadhi ya watumishi kutokataka kuambiwa ukweli kuhusu utendaji wao unaokwenda kinyume cha sheria za utumishi na kanuni za utumishi wa umma.

No comments: