Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Tuesday, November 15, 2011

Waasi 6 wa DRC waachiwa huru Kigoma

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma imewaachia huru na kuamuru kurudishwa nchini mwao waasisi sita wanaopinga Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) inayoongozwa na Rais Joseph Kabila, sambamba na kumuachia huru Nahodha wa boti moja ya mbao ambayo waasi hao waliitumia kuingia nayo nchini.

Akitoa hukumu mahakamani hapo, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa Kigoma, Emanuel Mrangu aliimbia Mahakama hiyo kwamba baada ya kupitia hati ya mashitaka, ushahidi wa mlalamikaji na maelezo ya utetezi ya washitaka ameridhika na mazingira ya kesi kuwaachia huru na kuamuru kurudishwa nchini mwao kwa waasi hao chini ya ulinzi wa vyombo vya ulinzi na usalama.


Aliwataja waasi hao walioamuriwa kurudishwa nchini kwao kuwa ni Masuku Omari, Samweli Kabwe, Maftaha Zuberi, Kasikilo Uledi, Vea Bumbenga na Kasikile Reti huku mahakamana hiyo ikimuacia huru Amuri Kiyombe nahodha wa boti hiyo ambaye ushahidi umethibitisha kuwa alitekwa na waasi hao na kulazimishwa kuwaleta nchini Tanzania kwa boti hiyo.


Aidha Mahakama hiyo imeahirishwa kutoa hukumu ya kiongozi wa waasi hao Kikanda Saidi aliyelazwa katika Hospitali ya Mkoa Kigomaya Maweni baada ya hali yake kuendelea kuwa mbaya na amepewa rufaa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi kufuatia kujeruhiwa vibaya wakati wa mapambano na wapiganaji wa Serikali ya Kongo.


Sambamba na hukumu hiyo Hakimu Mrangu ametoa tahadhari kuwa mpango wa kuwarejesha nchini mwao katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo waasi hao lifuate taratibu na itifaki zote za kimataifa kuhakikisha waasi hao wanakabidhiwa kwa mikono salama ya viongozi wa Serikali ya Kongo na wanatendewa kama binadamu.


Katika maelezo yake alisema, kwa kuwa watu hao wameasi Serikali ya Kongo wasije wakakabidhiwa katika namna ambayo itahatarisha maisha yao na kusababisha kuuawa jambo ambalo ni kinyume na haki za binadamu huku Tanzania ikiwa imeridhia kutekeleza haki za binadamu.


Wakitoa utetezi wao mahakamani hao waasi hao walikiri kuingia nchini wakiwa hawana nyaraka zozote za kusafiria za kuwaruhusu kuingia nchini jambo ambalo wanakiri kuwa kwa sheria za Tanzania walifanya kosa.


Hata hivyo walisema kuwa kabla ya kuondoka Kongo kuja Tanzania walipewa barua na viongozi wa ngazi za juu wa kundi hilo la waasi ikielezea kutambuliwa kwao na kupewa msaada kulingana na majeraha ya risasi waliyopata wakati wa mapambano na majeshi ya Serikali ya Kongo.


Awali ilielezwa mahakamani hapo na mwendesha mashitaka wa Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Kigoma, Gratian Lukoo kwamba Novemba 23, mwaka huu katika Bandari ndogo ya Kibirizi waasi hao walikamatwa kwa kuingia nchini wakiwa hawana kibali chochote kinachowaruhusu kuingia nchini jambo ambalo ni kosa kwa sheria ya uhamiaji.

No comments: