Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Tuesday, November 15, 2011

RC akemea wasiopeleka watoto kuchanjwa

MKUU wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya amekemea tabia ya baadhi ya wazazi na walezi mkoani humo kukaidi agizo la kuwapeleka watoto wao kupata chanjo cha magonjwa mbalimbali kwa kisingizio kwamba chanjo hiyo ina madhara kwa watoto wao.

Akizindua utoaji chanjo kwa ngazi ya mkoa katika Zahanati ya Msufini katika Manispaa ya Kigoma Ujiji juzi, Machibya alisema imani hiyo ya wazazi na walezi inayotokana na mila potofu, haina budi kupigwa vita na wazazi watumie nafasi hiyo kuwapeleka watoto wao kupata chanjo hiyo.


Alisema chanjo ya polio, surua, minyoo na Vitamini A ni muhimu kwa watoto chini ya miaka mitano mkoani Kigoma kutokana na muingiliano mkubwa uliopo mkoani humo kutokana na kupakana na nchi nne za ukanda wa Maziwa Makuu ambazo zimekuwa zikishambuliwa na ugonjwa wa polio mara kwa mara.


Alibainisha lengo la chanjo hiyo ni kutokomeza magonjwa hayo kwa watoto chini ya miaka mitano na kuzuia mlipuko wa surua na polio ili kulifanya taifa kuwa na watoto wenye afya njema na kuwa viongozi wa taifa hili katika siku za baadaye.


Awali, akisoma risala kwa Mkuu wa mkoa, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa, Amri Mulamuzi alisema watoto milioni 1.2 wanatarajia kupatiwa chanjo hiyo ambapo vituo 248 vinatarajia kuhusika katika utoaji wa chanjo hiyo miongoni mwao kukiwa na hospitali sita, vituo vya afya 24 na zahanati 223.


Kazi hiyo imeanza vizuri kwa idadi kubwa ya kinamama kujitokeza kupeleka watoto kupata chanjo hiyo, na mwandishi wetu alitembelea maeneo mbalimbali ya kutolea chanjo na kushuhudia ukiendelea bila matatizo.

No comments: