Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Tuesday, November 15, 2011

NCCR- Kama Zitto anataka kuja kwetu ruksa

CHAMA cha NCCR-Mageuzi kimesema kama Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto ana mpango wa kujiunga na chama hicho, anakaribishwa hata kama anataka kugombea nafasi ya uongozi milango ipo wazi.

Aidha, chama hicho kimekanusha taarifa zilizotolewa na baadhi ya magazeti kuwa Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia amepewa siku 21 za kujieleza pamoja na kuhusishwa na matumizi mabaya ya ruzuku ya Sh milioni 130 ambayo chama hupata kila mwezi.


Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samuel Ruhuza alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kwa lengo la kukanusha taarifa hizo kwa madai kuwa ni za mitaani zenye kupotosha na zilizojaa uchochezi.


Akizungumzia suala la Zitto kujiunga na chama hicho kama ambavyo baadhi ya magazeti yalivyokuwa yakiripoti, Ruhuza alisema chama hicho hakijapata taarifa zozote kuhusu hilo, lakini kama mbunge huyo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ana nia ya kufanya hivyo anakaribishwa.


“Zitto kama anataka kuja aje, hata kama anataka kugombea pia aje, hazuiliwi… na sio yeye peke yake, bali hata kama kuna mwananchi mwingine anayetaka kuja aje, chama hiki hakina mwenyewe na hamna mwenye hatimiliki, hakina mmiliki,” alisema Ruhuza wakati akijibu maswali ya wanahabari.


Kuhusu taarifa za upotoshaji, alisema ni kweli chama hicho kilikuwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa Novemba 5, lakini jambo la kushangaza bila kushirikisha wanahabari katika kikao hicho, kesho yake wakaona taarifa ambazo hazikuwa na ukweli wowote.


Alisema kimsingi taarifa hizo ni za kupotosha umma, zilizojaa uchochezi zinalenga kukichafua chama na tayari zimesababisha madhara makubwa kwani hata wafadhili wao wameshindwa kuchangia wakijua wazi kuwa chama kina ruzuku ya kiwango hicho. Hakutaja kiwango halisi cha ruzuku wanachopata.


Hata hivyo, Ruhuza alisema kutokana na hali hiyo, vyombo vya habari vilivyoripoti taarifa hizo, chama kitavifuatilia kisheria ili vithibitishe taarifa zao.

No comments: