Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Friday, November 25, 2011

Viongozi wa kijiji wawasuta Wabunge wa Kasulu

WABUNGE wa NCCR-Mageuzi, Moses Machali (Kasulu Mjini) na Agripina Buyogera (Kasulu Vijijini), wanadaiwa kutoa maelezo ya uongo bungeni na taarifa za uongo kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, juu ya kuuawa kwa watu wawili na sita kubakwa wakati wa kuwaondoa waliovamia Hifadhi ya Msitu wa Makere wilayani Kasulu hivi karibuni.

Uongozi wa Serikali ya Kijiji na wananchi wa vijiji vya Kagera Nkanda na Mvinza, walithibitisha hayo juzi mbele ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, aliyetumwa wilayani humo na Waziri Mkuu kufuatilia na kuhakiki usahihi wa taarifa hizo walizotoa wabunge hao kwa kiongozi huyo wa Serikali.


Akitoa ushuhuda kuhusu madai hayo ya wabunge mbele ya umati wa wananchi wa kijiji cha Kagera Nkanda, Mjumbe wa Serikali ya Kijiji hicho, Majaliwa Ramadhani, alisema hakuna ukweli wowote juu ya taarifa hizo na kwamba kilichoelezwa na wabunge hao ni uzushi.


Majaliwa alisema kazi ya kuwaondoa wavamizi katika maeneo ya hifadhi ilikuwa ya wazi na shirikishi na hakuna mwananchi anayeweza kuthibitisha mauaji na ubakaji wakati wa kazi hiyo.


Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Francis Mtibiro, alisema hakuna taarifa yoyote ambayo ilitolewa kwao na wananchi waliokuwa wakilima katika maeneo hayo kuhusu mauaji na ubakaji, kwani alisema hata nyumba zinazodaiwa kuchomwa, ni vibanda vya nyasi vilivyojengwa kwa ajili ya kujikinga mvua.


Baada ya mkutano huo, msafara wa Waziri Maige ulikwenda Mvinza ambako wananchi wa kijiji hicho, Teamili Ntirubaza, Shukuru Modesto na Norbert Revocatus, walimweleza, kwamba taarifa za mauaji na ubakaji alizopewa Waziri na kumfanya kufika kijijini hapo kupata uhakika, ni uongo mtupu.


Mbali na kukanusha taarifa hizo, wananchi hao walitoa ombi kwa Waziri la kutaka kuongezwa eneo kwa ajili ya kilimo na kuepusha mgogoro wa kutojua mipaka, jambo ambalo limefanya baadhi yao kuingia kulima eneo la hifadhi.


Wakati wote wananchi hao wakitoa ushuhuda huo, hakuna Mbunge kati ya hao wawili, aliyechangia chochote na ajenda hiyo haikuwa yao wala kutoa msaada kueleza yale waliyomweleza Waziri Mkuu.


Awali kabla ya msafara wa viongozi haujaondoka Kasulu kwenda eneo la tukio, wabunge hao walishikilia msimamo wao, kwamba wana taarifa za uhakika baada ya kupigiwa simu na ujumbe mfupi wa simu ya mkononi, kueleza kuwapo mauaji na ubakaji wakati wa kuendesha operesheni hiyo.


Waziri Maige akihitimisha siku ya kwanza ya ziara yake ya siku mbili Kasulu, alihutubia mkutano wa hadhara mjini humo na kuwataka wabunge hao kuwa wakweli wanapotoa taarifa kwa viongozi na kuzifanyia kazi taarifa wanazopewa, badala ya kukurupuka.


Aidha, katika mkutano huo wa hadhara Kasulu, wabunge hao walikiri kuwa walimpa taarifa za uongo Waziri Mkuu, wakiwa hawajazifanyia utafiti wa kina, baada ya kuzipokea kwa njia ya simu kutoka kwa wapiga kura wao.


Kutokana na hali hiyo, Machali alitangaza kubadilisha utaratibu wa wapiga kura kuwasiliana naye na kupiga marufuku mwananchi yeyote kumpigia simu wala kutuma ujumbe mfupi wa maandishi, kumweleza shida na matatizo yao, badala yake wawasiliane naye ana kwa ana na kwa barua kupitia kwa Katibu wake.


Buyogera alisema unafiki wa wananchi wa jimbo lake, ndio umewafikisha viongozi hao hapo na kuonekana waongo mbele ya jamii na kuwataka kuacha kufanya jambo hilo tena.


Akihitimisha ziara hiyo ya kuzungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Danhi Makanga, alisema kazi ya kuwaondoa wavamizi kwenye hifadhi ni endelevu na yeyote atakayekamatwa huko atachukuliwa hatua kali za kisheria.


Hivi karibuni, wakati wa kikao cha Bunge, wabunge hao walitoa maelezo bungeni sambamba na kumpa taarifa rasmi Waziri Mkuu, kuhusu mauaji ya watu wawili, kubakwa kwa wengine sita na nyumba ambazo idadi yake haijulikani kuchomwa moto, wakati wa kuwaondoa wavamizi kwenye msitu wa Hifadhi wa Makere.


Kutokana na taarifa hizo, Waziri Mkuu alimwagiza Waziri Maige na Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki, Dk. Felician Kilahama na baadhi ya wataalamu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, kwenda Kasulu kufuatilia taarifa hizo na kumpa maelezo ya kina ya kilichofanyika.

No comments: