Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Wednesday, November 2, 2011

RC- Usafi Kigoma iwe ajenda ya kudumu

MKUU wa Mkoa Kigoma, Issa Machibya amezindua maadhimisho ya sherehe za miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara katika mkoa huo na kutoa agizo kuwa suala la usafi wa mji huo, liwe ajenda ya kudumu kwa viongozi na wananchi.

Machibya alisema hayo mjini Kigoma jana katika hafla ya maadhimisho hayo iliyofanyika kwenye soko la wakulima Nazareth. Alisema hali ya mji huo kwa sasa inatisha na hatua za makusudi za kuufanya kuwa safi wakati wote hazina budi kuchukuliwa.


Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya Kigoma, John Mongela alisema bado viongozi wa Serikali, taasisi zisizo za Serikali na jamii hawajaona umuhimu wa kuuweka mji wao katika hali ya usafi.


“Hatuwezi kwenda namna hii kila mahali ukipita mji unanuka utadhani hakuna watu, hakuna viongozi, ni lazima tubadilike kila mmoja kwa nafasi yake ajipe jukumu la kuwa msimamizi wa mwenzake katika utekelezaji wa kuweka mji katika hali ya usafi,” alisema.


Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, walitaka agizo hilo lisiwe la nguvu za soda badala yake usimamizi wa karibu uwepo kwa kuwashirikisha wananchi katika kutekeleza hilo.


Mmoja wa wananchi hao, Babu Pascal ambaye ni Mratibu wa Shirika la Maendeleo ya Vijana Kigoma (KIVIDEA), alisema kuwa viongozi na wananchi wanapaswa kumuunga mkono Mkuu wa Mkoa katika kuufanya mji wa Kigoma Ujiji kuwa safi.


Pascal alisema kuwa wakati mwingine inatia aibu wanapokuja wageni na kukuta kila eneo la mji huo linanuka huku kukiwa hakuna uwajibikaji wa dhati wa viongozi katika kuondoa hali hiyo.

No comments: