Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Wednesday, November 2, 2011

Makandarasi waidai Serikali bilioni 425/- alisema Serukamba ambaye ni Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM).

MAKANDARASI wa barabara wanaidai Serikali zaidi ya Sh bilioni 425/-

Kutokana na deni hilo, ujenzi wa barabara 11 umesimama na nyingine zinajengwa kwa kusuasua, Bunge limetanabaisha.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa ya ujenzi wa barabara nchini iliyowasilishwa na Wizara ya Ujenzi, Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Peter Serukamba, alisema kamati yake inaagiza hatua za haraka zichukuliwe.

Serukamba alisema, kwa mujibu wa ripoti hiyo, imebainika kutokana na deni hilo, miradi 11 ya barabara ambayo ni barabara ya Sumbawanga-Kanazi, Kanazi-Kizi-Kibaoni, Lwanjilo- Chunya, Bariadi-Lamadi na Kagoma-Lusahunga imesimama kujengwa.

Miradi mingine iliyosimama kujengwa ni barabara ya Tabora-Ndono, Ndono-Urambo, Jet Corner -Vituka-Davis Corner, Ubungo Terminal-Kigogo-Kawawa na Kawawa-Msimbazi-Twiga.

Aidha, alisema pia kutokana na tatizo hilo, miradi mingine sita imekuwa ikijengwa kwa kusuasua ambayo ni Marangu-Rombo Mkuu, Sumbawanga-Kasanga, Magole-Turiani, Korogwe-Handeni, Kagoma-Lusahunga na Isaka-Ushirombo.

Alisema, pia tayari makandarasi wa miradi saba wametoa notisi ya kusimamisha ujenzi iwapo hawatolipwa na miradi hiyo ni Singida-Katesh, Kitumbi-Segera-Tanga, Bagamoyo-Msata, Mkata-Handeni, Nzega-Puge, Tabora-Nyahua na Mwanza-Musoma.

Mwenyekiti huyo alisema, katika miradi hiyo, ipo ambayo mikataba yake inaonesha kuwa kwa siku makandarasi wanalipwa Sh milioni 800 sawa na Sh bilioni 2.5 hivyo kushindwa kuendelea na kazi.

“Lazima Serikali hata kwa kukopa itafute fedha hizi, Kamati yangu itakutana na Waziri Mkuu pamoja na Waziri wa Fedha kuzungumzia suala hili kwani tukiliacha maana yake deni hili litazidi na miradi hii itakufa,” alisema Serukamba ambaye ni Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM).

Kuhusu tatizo la bomoabomoa linaloendelea nchini, kamati hiyo imeshauri Wizara iangalie uwezekano wa kukutanisha idara zote zinazohusiana na suala hilo ili sheria ziangaliwe kwa mapana na kupunguza migogoro.

Alisema ni vyema viwanja vinavyopimwa kuanzia sasa vitenge maeneo ya umeme, maji na huduma nyingine muhimu.

No comments: