Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Friday, November 11, 2011

Polisi wataja sababu za kuingia silaha nchini

POLISI mkoani Kigoma imesema ukubwa wa mipaka ya Tanzania na nchi jirani, uhaba wa vitendea kazi na uchache wa askari waliopo hapa kwa ajili ya ulinzi wa mpaka huo ni miongoni mwa changamoto zinazochangia watu wasio na nia njema kuingiza silaha zinazotumika kwenye matukio ya ujambazi nchini.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Fraiser Kashai alisema hayo wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu kukamatwa kwa bunduki na idadi kubwa ya risasi katika matukio ya mwishoni mwa wiki.


Kamanda Kashai alisema kazi ya kulinda mipaka ni ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, lakini ukubwa wa mpaka wa Tanzania na nchi za Maziwa Makuu, unaruhusu kuwepo kwa njia nyingi za panya ambazo hutumiwa na watu wasio wema katika kuingiza silaha haramu nchini.


Alisema kwa upande wao, wanakabiliwa na uhaba wa vitendea kazi vya kufanya doria ikiwemo magari ambavyo havitoshelezi kufanya kazi kwa namna jeshi hilo linavyotaka na kwamba suala la bajeti hasa upatikanaji wa mafuta ya kutosha kwa ajili ya doria ni changamoto kubwa kwao.


Hata hivyo, alisema pamoja na changamoto hizo, jeshi hilo limekuwa likifanya kazi kufa au kupona katika kuhakikisha kunakuwepo na hali ya ulinzi na usalama wa raia na mali zao na kufanya upekuzi katika vituo mbalimbali kwa njia zinazoingia na kutoka mkoani humo.


Akitoa taarifa ya kukamatwa kwa silaha, Kamanda Kashai alisema bunduki tatu aina ya SMG, gobori moja na risasi 394 za bunduki aina ya SMG vimekamatwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kigoma.


Mbali na kukamatwa kwa silaha hizo, Kamanda alisema watu wanne wametiwa mbaroni kwa kuhusika na silaha hizo, lakini pia wakidaiwa kuhusika na mtandao wa uuzaji wa silaha mkoani humo.


Aliwataja watu waliokamatwa kuwa ni Majaliwa Emmanuel (20) mkazi wa Kijiji cha Kumwerulo, Christopher John (26) na Yoram Vincent; wote wakazi wa Kijiji cha Nengo mjini Kibondo na Evarist Nyamtama anayeishi Kalinzi Kigoma Vijijini ambaye alikamatwa Nguruka.

No comments: