Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Wednesday, November 9, 2011

Askari wanane waasi wa DRC kizimbani Kigoma

ASKARI wanane wa Jeshi la Waasi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) wamefikishwa mahakamani mjini hapa na kusomewa mashitaka mawili ya kuingia nchini bila vibali na kumiliki silaha isivyo halali.

Katika shitaka la kwanza, Mwendesha Mashitaka kutoka Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Kigoma, Rogasian Lukoo alisema Novemba 3, mwaka huu katika bandari ndogo ya Kibirizi, Kikanda Saidi na watuhumiwa wenzake sita, waliingia nchini bila kuwa na kibali chochote kinachowaruhusu kuingia na kuishi nchini.


Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa, Emmanuel Mrangu, Mwendesha Mashitaka huyo alidai watuhumiwa wamesomewa mashitaka yao chini ya kifungu cha 31 (1) na 7 cha mwaka 2005 na kifungu cha 54 cha marekebisho ya mwaka 2004.


Waliosomewa mashitaka ni Masuku Omari, Samweli Kabwe, Maftaha Zuberi, Kasikilo Uledi, Vea Bomba, Kiombela Omari na Saidi (Meja) aliyesomewa mashitaka yake kitandani katika Hospitali ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni ambapo hata hivyo watuhumiwa hao walikana shitaka lao.


Katika utetezi wao, watuhumiwa hao, walidai wakati wanatoka Congo kuja nchini Tanzania, walikuja na barua kutoka kwa viongozi wao wa kikundi chao kinachojulikana kama Kikundi cha Ukombozi na Maendeleo kinachopinga utawala wa Rais Joseph Kabila wakiomba kupatiwa matibabu nchini.


Kiongozi wa kikundi hicho, Saidi alidai badala ya kupatiwa matibabu kama ambavyo barua yao inaeleza wamejikuta wakikamatwa na kufunguliwa mashitaka ya kuingia Tanzania isivyo halali.


Aidha, mmoja wa waasi hao, Shabani Kambi aliyejeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili, alifariki dunia juzi hospitalini hapo wakati akiendelea kupata matibabu na taratibu za mazishi yake zinaendelea huku mwili wake ukiwa umehifadhiwa Hospitali ya Mkoa wa Kigoma.


Mwendesha Mashitaka aliieleza kuwa upelelezi juu ya shauri hilo umekamilika na kumuomba hakimu kupanga tarehe ya kuanza kusikilizwa na kutokana na unyeti wake. Hakimu alisema itaanza kusikilizwa leo.


Mbali na shitaka la kuingia nchini isivyo halali, pia watuhumiwa hao walisomewa mashitaka ya kumiliki na kuingia na bunduki, risasi na mizinga ya kutungulia ndege isivyo halali wakati wakijua kufanya hivyo ni kosa.


Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Amoni Challe alidai kuwa Novemba 3, mwaka huu saa tatu asubuhi katika Kijiji cha Mtanga mwambao wa kaskazini wa Ziwa Tanganyika wapiganaji hao wa kikundi cha Mayi Mayi walikamatwa wakiwa na silaha mbalimbali ambazo walikuwa wakizimiliki isivyo halali.


Challe alidai watuhumiwa hao walikamatwa na askari wa JWTZ katika kijiji hicho cha mpakani baada ya kujisalimisha wakiomba kupatiwa matibabu kutokana na majeraha mbalimbali ya risasi yaliyokuwa nayo.


Alidai upelelezi wa kesi hiyo unaendelea na kumuomba Hakimu Mrangu kupanga siku nyingine ya kesi hiyo kuitwa mahakamani hapo ambapo mahakama imeahirisha hadi Novemba 21, mwaka huu.


Katika hatua nyingine, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limesema linaendelea kuwahoji askari 20 wa kikosi maalumu cha Jeshi la Ulinzi la DRC kwa kuingia nchini na silaha za kivita bila kutoa taarifa.


Msemaji wa JWTZ, Luteni Kanali Kapambala Mgawe aliliambia gazeti hili jana Dar es Salaam kuwa wanajeshi hao wanashikiliwa na Polisi Kigoma wakitakiwa kujibu sababu iliyowafanya kuingia nchini katika hali hiyo.

No comments: