Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Tuesday, November 15, 2011

Kigoma yatafuta mbadala wa tumbaku

MKOA wa Kigoma umeanza uhamasishaji wa kilimo cha ufuta na alizeti kama mazao makuu ya biashara ikiwa mbadala wa kilimo cha tumbaku ambalo limekuwa na matatizo ya bei katika soko la dunia pamoja na athari katika uharibifu wa mazingira.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya alizindua uhamasishaji huo juzi jioni katika Mji Mdogo wa Nguruka, Kigoma Vijijini kwa kugawa mbegu za ufuta kwa wakulima zaidi ya 200 waliojitokeza kuanza kulima mazao hayo katika msimu huu wa kilimo.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa uhamasishaji huo, Machibya alisema ufuta na alizeti ni mazao ambayo kwa sasa yana soko kubwa la uhakika duniani na yamekuwa yakihitajika sana na kuomba wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi katika kushiriki kwenye kilimo hicho.


Alisema mazao hayo mawili kwa sasa yatakuwa mbadala wa zao la tumbaku ambalo limeanza kuleta athari kubwa katika suala zima la kimazingira kutokana na ukataji mkubwa wa miti ambayo hutumika katika kukaushia tumbaku, lakini upandaji wa miti kwa wakulima wa zao hilo umekuwa wa kiwango kidogo.


Mbali na uharibifu wa mazingira, lakini pia alisema tumbaku imekuwa ikiathiri afya za wakulima na watu mbalimbali wanaohusika na ulimaji, uvunaji na ukaushaji wa zao hilo kutokana na hewa ya nicotin wanayovuta ambayo husababishwa na tumbaku.


Katika kuhakikisha mazao hayo yanapata mafanikio, alisema mkazo utawekwa kuhakikisha wakulima wanapatiwa pembejeo, zana za kilimo na wataalamu wa kilimo wamepewa jukumu la kutafuta masoko kwa ajili ya mazao hayo ili kuondoa usumbufu kwa wakulima katika kupata soko.


Awali, Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Daniel Kamwela alisema wakulima 210 wameshajitokeza hadi sasa kwa ajili ya kuanza kulima ufuta na alizeti katika Wilaya ya Kigoma na mbegu za kilimo 750 zimepokelewa kama mbegu ya ufuta kwa wakulima wa wilaya hiyo.


Kamwela alisema idara yake imejipanga katika kuhakikisha kuwa wakulima wanapatiwa mbegu bora na utaalamu wa kilimo hicho sambamba na kuweka mkakati wa utafutaji wa masoko.

 
     

No comments: