Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Tuesday, November 22, 2011

Mapadri 4 wafa ajalini Pwani, alikuwa wanatoka Kigoma kwenda Dar es Salaam

MAPADRI wanne wamekufa papo hapo baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na lori eneo la Ruvu kwa Zoka, Bagamoyo mkoani Pwani.

Ajali hiyo ilitokea jana mchana baada ya gari aina ya Toyota Land Cruiser namba T903ACQ mali ya Parokia ya Pugu, Dar es Salaam, lililokuwa likiendeshwa na Sylverio Ghell, mkazi wa Pugu, kugongana uso kwa uso na lori hilo.


Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Ernest Mangu, ajali hiyo ilitokea baada ya gari hilo lililokuwa likitoka Kigoma kwenda Dar es Salaam kutaka kulipita lori mbele yake namba T181 BSQ na tela namba T286 ASY, na kugongana na lori namba T648 AET na tela namba T975 AYN.


Kamanda Mangu alitaja waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni Ghell, Corrab Trivelli, Lucino Baffivi na mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Andrew, wote raia wa Italia.


Mapadri hao ni wa Shirika la Wafrancisco Wakapuchini ambao baadhi yao hufanya kazi nchini.


Alieleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa gari la mapadri hao, likitaka kupita gari lingine. Maiti wote wamehifadhiwa katika Hospitali Teule ya Tumbi, Kibaha, Pwani.


Hata hivyo Mkuu wa Shirika la Wafrancisco Wakapuchini, Padri Wolfan alisema mapadri waliokufa ni watatu waliokuwa wakitoka Kongwa, Dodoma kwenda Dar es Salaam. Hata hivyo simu yake ilikatika na hakupatikana tena kutoa ufafanuzi zaidi.


Wakati huo huo, Gloria Tesha anaripoti kwamba wanafunzi sita wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) waliokuwa wakisoma Shahada ya Uzamili ya Hisabati ni miongoni mwa abiria 18 waliopoteza maisha katika ajali ya basi la Taqwa lililotokea Jumamosi mkoani Kagera.


Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Rusahunga, wilayani Biharamulo na abiria 17 walijeruhiwa wakiwamo wanafunzi wanne wa UDSM. Wanafunzi waliokufa, wawili ni Watanzania na wengine wanatoka Uganda, Malawi na Zambia.


Awali, baada ya ajali hiyo, gazeti hili liliripoti kuwa mwanafunzi na mhadhiri wa chuo hicho ni miongoni mwa waliokufa katika ajali hiyo.


Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala, aliwataja wanafunzi waliokufa na nchi zao kwenye mabano kuwa ni Kassim Dadi, Mhadhiri Msaidizi wa Idara ya Hisabati UDSM na Nshaija Muganyizi (Tanzania), Mubiru Patrick (Uganda), Chikondi Chasowa na Josephine Kaleso (Malawi) na Chimuka Hamajata (Zambia).


Mukandala katika taarifa yake kwa vyombo vya habari juzi jioni, alisema waliokufa walikuwa katika kundi la wanafunzi 10 wa kimataifa wanaosoma Hisabati katika chuo hicho na walikuwa wakienda Kigali, Rwanda, kwa ziara ya kimasomo kwenye Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Kigali (KIST).


“Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Rwekaza Mukandala anasikitika kueleza kuwa katika ajali hiyo, wanafunzi sita wamepoteza maisha, hili ni kundi la wanafunzi wa kimataifa waliokuwa wakisoma Shahada ya Uzamili ya Hisabati chini ya Programu ya Hisabati ya Vyuo Vikuu vya Mashariki mwa Afrika (EAUMP),” ilieleza taarifa hiyo.


Ofisa Habari wa UDSM, Jackson Isdory, aliliambia gazeti hili jana, kuwa utaratibu wa maziko unategemea uamuzi wa ndugu wa marehemu, ili chuo kitekeleze sehemu yake kulingana na sera zake, ikiwa ni pamoja na kugharamia mazishi.


“Muganyizi anatarajiwa kuzikwa leo (jana) Bukoba, na ujumbe wa chuo umekwenda pamoja na mkewe na taarifa za muda mfupi zimebainisha kuwa wa Uganda amesafirishwa leo (jana) kutoka Kagera baada ya taratibu za uhamiaji kukamilika,” alisema Isdory.


Alisema Kampuni ya Taqwa ilisafirisha jana maiti na majeruhi kupelekwa Dar es Salaam, ambako ndugu kwa kushirikiana na uongozi wa chuo, wataendelea na utaratibu wa maziko na majeruhi kupelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu na uangalizi zaidi.


Kwa mujibu wa Isdory, wanafunzi waliojeruhiwa wote ni Watanzania na majina yao ni Rose Mara, John Andonywisye (aliyedaiwa kufa awali), Mwale Moses na Samnya Suleimani, ambaye hakuumia na ndiye aliyetoa taarifa kwa simu chuoni kuhusu ajali na vifo vya wenzake baada ya tukio.


Ajali hiyo iliyotokea Jumamosi asubuhi, ilihusisha basi la abiria la Kampuni ya Taqwa namba T635ABC aina ya Nissan Diesel lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Bujumbura, Burundi na lori la Kampuni ya Bakhresa namba RAB255ACT lililokuwa likitoka Ngara kwenda Dar es Salaam.


Awali, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Henry Salewi, aliwataja waliokufa kuwa ni Hamajata, mwanafunzi wa UDSM na raia wa Zambia anayeishi Kitwe, dereva wa basi hilo, Sultan Mohamed (36), mwenyeji wa Kahama, Shinyanga; dereva wa lori Ruzindana Theonest (35) na abiria wengine 15.


Alisema chanzo cha ajali ni uzembe wa madereva wote wawili. Kamanda Salewi alisema majeruhi waliolazwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Biharamulo na Hospitali ya Omurugwanza wilayani Ngara ni 17 na watano hali zao ni mbaya.

No comments: