Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Tuesday, October 11, 2011

Ziara ya Chiza yagubikwa na malalamiko Kigoma

ZIARA ya Naibu Waziri wa Chakula, Kilimo na Ushirika, Christopher Chiza mkoani Kigoma imegubikwa na malalamiko ya wakulima kwamba wafugaji kutoka Shinyanga wamevamia mashamba yao na kuyageuza malisho ya mifugo. 


Wakizungumza katika mikutano ya hadhara maeno mbalimbali ya mkoa huo, wakulima hao walisema kuwa pamoja na kutoa taarifa za vitendo hivyo vya wafugaji, malalamiko yao hayafanyiwi kazi.


Bernad Ntabega; mkulima katika kijiji cha Rungwe Mpya wilayani Kasulu, alisema wafugaji hao wamekuwa na jeuri ya kujibu na kufanya chochote kutokana na uwezo wao wa kifedha.


Alidai kuwa hata taarifa zinapotolewa Polisi hakuna hatua zozote zinazochukuliwa.


Naye Ems Juma alimwambia Naibu Waziri kwamba viongozi wa vijiji ni tatizo kubwa na wafugaji hao wanapoulizwa wanabainisha kwamba wamepewa vibali na viongozi wa vijiji baada ya kutoa fedha nyingi ili kupewa maeneo hayo.


Kutokana na hali hiyo Naibu Waziri huyo alipiga marufuku viongozi wa vijiji na vitongoji kutoa vibali vya kuruhusu wafugaji kuingia katika maeneo ya vijiji na kutaka vibali hivyo vitolewe na mkuu wa wilaya.


Alisema kuwa zipo taratibu za kisheria zilizowekwa kwa ajili ya wafugaji wahamiaji kuingia vijijini na kupewa maeneo kwa ajili ya mifugo yao na kutaka taratibu hizo zifuatwe na pale viongozi wa vijiji watakapoonekana wamechukua uamuzi mbaya washughulikiwe kwa mujibu wa sheria.

No comments: