Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Tuesday, October 11, 2011

Vinavyochangia kuwepo kwa uhalifu Kigoma vyabainishwa

MKUU wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya amesema serikali haipo tayari kuona amani ikipotea na wananchi wakiishi kwa hofu kutokana na kukithiri kwa matukio ya uhalifu yanayosababishwa na uingizwaji silaha kutoka nje.


Machibya alisema hayo wakati akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Kasulu baada ya kutembelea mpaka wa Tanzania na Burundi katika kijiji cha Mnanila.

Alisema Serikali itafanya kila jitihada ili kukomesha vitendo vya uhalifu na kuwawezesha wananchi kufanya shughuli zao kwa amani.

Machibya alisema Serikali haikuwa tayari kuona wananchi wakipata shida na kushindwa kufanya kazi za maendeleo kwa sababu za kuwepo kwa wakimbizi ambao wanavunja sheria.

Awali Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Dahn Makanga alieleza kuwa ukubwa wa mpaka na nchi jirani ya Burundi na uhaba wa vitendea kazi, umechangia kupitishwa kwa magendo na silaha haramu na kuhatarisha usalama pamoja na kuikosesha Serikali mapato.

Alisema kuwepo kwa kambi za wakimbizi kutoka Burundi na Congo DRC kumesababisha kuongezeka kwa uhalifu na mpango wa sasa wa Serikali na mashirika yanayotoa huduma kwa
wakimbizi, ni kuyafunga makambi yote.

Alisema kambi ya wakimbizi kutoka Burundi ya Mtabila yenye karibu wakimbizi elfu arobaini, itafungwa Desemba 31, mwaka huu na ile ya Nyarugusu ya wakimbizi kutoka Congo DRC, itafungwa Machi mwakani.

 

No comments: