Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Thursday, October 6, 2011

Ukanda wa Ziwa Tanganyika wafungua uwekezaji Kigoma

“Ukanda wa Ziwa Tanganyika unaohusisha mikoa ya Kigoma na Rukwa na mkoa mpya wa Katavi, umekuwa ukijulikana kama Ukanda wa mikoa ya pembezoni mwa Tanzania, ukisifika kwa miundombinu duni ya huduma za kiuchumi na kijamii”, anasema Mkuu mpya wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Stella Manyanya.

Anasema tangu enzi za ukoloni, maeneo hayo yalikuwa yameachwa maalum kama sehemu ya akiba ya nguvu kazi ya mashamba ya mikonge na shughuli nyingine.


Manyanya anasema hali hiyo ilisababisha kusahaulika katika harakati za maendeleo ya mawasiliano ya barabara, usafiri wa majini yaani bandari, reli, usafiri wa ndege pamoja na mawasiliano ya simu, runinga na redio.


Sababu zingine ni eneo hili kuwa nje ya Gridi ya Taifa ya Umeme, hivyo kukosa umeme wa uhakika hali iliyosababisha kuwa ukanda wenye mazingira magumu ya uwekezaji ingawa unao utajiri mkubwa wa rasilimali ambazo hazijatumika.


Anasema lakini katika Serikali ya awamu ya nne, kazi kubwa ya kuufungua ukanda huu imefanyika katika ujenzi wa miundombinu ya barabara za lami, viwanja vya ndege, bandari katika Ziwa Tanganyika, uimarishaji wa upatikanaji wa umeme pamoja na kuboresha

huduma za jamii.

Anasisitiza kuwa mabadiliko hayo yanatokana na juhudi za serikali hayawezi kuwa na tija

iwapo miundombinu hiyo haitaweza kutumika kupeleka maendeleo iwapo haitatangazwa na
kuanza kutumika kwa wananchi na wawekezaji wengine.

Kutokana na kufunguka kwa mawasiliano, Manyanya kwa niaba ya wakuu wa mikoa mingine ya

kanda hiyo anawaalika wawekezaji kuwekeza katika mikoa hiyo yenye vivutio mbalimbali huku akiwasihi wawekezaji wa ndani kujitokeza.

“Tumeweka mipango ya wale wenye uwezo mkubwa wa fedha na mdogo hivyo kila mmoja ana nafasi ya kuwekeza katika ukanda huu bila kusubiri wawekezaji wa nje.”Anasisitiza. Anasema vipaumbele vya uwekezaji wa ukanda huo ni pamoja na rasilimali watu.


Anasema kuwa katika Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2002, ukanda huo ulikuwa na watu 2,180,390 na mwaka huu unakisiwa kuwa na watu 3,225,264. Ongezeko la watu ni la asilimia 3.5 kwa mwaka.


Anasema idadi hiyo ni soko zuri la bidhaa yoyote inayozalishwa katika ukanda huu. Soko hili hukua zaidi linapounganishwa na idadi ya watu katika nchi za Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Burundi. Inakadiriwa kuwa asilimia 40 ya wakazi hao ni

wachapakazi.

Anasema katika kilimo, ufugaji na uvuvi, ukanda huo una eneo la kilometa za mraba 120,315, ambapo kilometa za mraba 15,157 ni eneo la maji na kilometa 34,453 ni Hifadhi za Misitu na Mbuga za wanyama.


Manyanya anasema kilometa za mraba 70,655 ni eneo la ardhi, linalotumika kwa ajili ya makazi, kilimo, ufugaji na uchimbaji wa madini ambapo zaidi ya asilimia 70 ya eneo hilo halijaanza kutumika hadi sasa.


Ukanda wote wa ziwa Tanganyika, una ardhi na hali ya hewa nzuri kwa kilimo huku mvua ikinyesha kwa wastani wa 600mm hadi 1100mm kwa mwaka, hali ambayo ni kivutio cha kuwekeza katika kilimo.


“Zipo ranchi tatu za Nkundi, Uvinza na Kalambo na kiwanda cha kusindika nyama kwa ajili ya kuuza nje ya nchi, kinachohitaji wawekezaji katika shughuli za mifugo ili kukipatia malighafi kwa ajili ya uzalishaji”, anasema Manyanya.


Pia, vipo viwanda vya kusindika unga wa mahindi na viwanda vidogo vya ukamuaji wa mafuta ya alizeti, mawese na kutengeneza sabuni. Kuna wakulima wakubwa na wadogo wanaomiliki ardhi na wapo tayari kuingia ubia na wawekezaji wenye mapenzi mema wa ndani na nje ya ukanda huo.


Ukanda huo una maziwa makubwa mawili ya Tanganyika na Rukwa, ambayo ni maarufu kwa

uvuvi wa samaki. Ziwa Tanganyika ni kiungo kikubwa cha wakazi wa Ukanda huo pamoja na nchi jirani za Zambia, DRC na Burundi.

Akizungumzia utalii, anasema vipo vivutio vya utalii katika mbuga za wanyama za Katavi, Mahale na Gombe na maeneo ya kihistoria ya kumbukumbu ya Dk. David Livingstone na Meli ya Mv Liemba.


Meli ya Mv Liemba ilifanya kazi zaidi ya miaka 100 iliyopita na kushiriki katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia na inafanya kazi hadi sasa. Aliwataka wawekezaji wenye uzoefu na biashara za kitalii kujenga hoteli katika miji ya ukanda huo na katika mbuga za hifadhi.


Anasema ukanda huo una shughuli nyingi za kitalii, kama uwindaji, upigaji picha na shughuli za kihistoria. Anasema ukanda huo unayo madini mengi, kama vile makaa ya mawe, shaba, dhahabu, chokaa na mengineyo, ambayo bado hayajaanza kuchimbwa kwa manufaa ya nchi.


Akizungumzia uwekezaji katika viwanda na biashara, anasema serikali imeboresha bandari za Kasanga na Kigoma, hivyo uwekezaji unahitajika kutoa huduma za usafiri wa meli za abiria, meli za uvuvi na viwanda vya usindikajiwa wa samaki.


“Kutokana na uzalishaji wa mahindi, mpunga, alizeti na mawese ipo fursa ya kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kusindika mazao,” anasema.


Anasema fursa nyingine za uwekezaji wa miundombinu ya kijamii na kiuchumi ni katika ujenzi wa vyuo vya ufundi, kilimo, elimu na vyuo vikuu na ujenzi wa hospitali kubwa za rufaa na kujenga vinu vya kuzalisha umeme katika maeneo mengi ya ukanda huo, kama maporomoko ya Kalambo na Ntembo wilaya ya Nkasi.


Manyanya anatoa wito kwa kwa wamiliki wa ndege, ambao wangependa kutoa huduma za usafiri kuanzisha huduma ya kihistoria ya usafiri wa ndege katika ukanda huo, kufanya hivyo.

Pia, anasema yapo mabonde makubwa yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, yaliyo wazi na wanayohitaji wabia.

Manyanya anasema ukanda huo umeandaa mkutano wa uwekezaji katika ukanda huo, utakaofunguliwa Oktoba 16 mwaka huu na Rais Jakaya Kikwete. Utafanyika Mjini Mpanda.

Anasema ujumbe wa mkutano huo utakuwa ‘Unleash the Investment Potential of Lake Tanganyika’.

Kutakuwa na mabanda ya maonesho katika eneo la mkutano kuanzia Oktoba 15 hadi 18 mwaka huu. Mabanda hayo yataonesha vivutio mbalimbali vilivyopo katika ukanda huo na mafanikio waliyoanza kupata katika uwekezaji.


Mazingira ya mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma yanafanana katika sekta nyingi, ikiwemo yote ni mikoa ya pembezoni, yaani mpakani mwa ziwa Tanganyika. Ni mipaka ya nchi za Zambia, DRC, Rwanda na Burundi.


Pia, anasema mila na desturi za wakazi wa mikoa hii, zinalandana huku miundombinu inayounganisha mikoa hii ni duni, hususan barabarani. Manyanya anasema watafanyia

mkutano huo mjini Mpanda kwa sababu ni makao makuu ya mkoa mpya wa Katavi, wenye vivutio vingi na rasilimali nyingi muhimu ambazo hazijatangazwa.

Washiriki wengi wataona vivutio hivyo na kuona rasilimali hizo na watazitangaza watakaporudi kwao.


Anasema maandalizi ya mkutano huo, yanaenda vizuri na tayari wameandaa vipeperushi na vijarida vinavyoonesha maeneo yenye vivutio na uwekezaji kwenye ukanda huo wa Ziwa Tanganyika; na pia wametengeneza filamu, inayoonesha fursa za uwekezaji zilizomo katika ukanda huu.


Pia, wamekwishaandaa tovuti ya ukanda huo.

No comments: