Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Thursday, October 6, 2011

Kilimo Kwanza kutekelezwa Bonde la Kagera

SERIKALI inatarajia kuanzisha mradi mkubwa wa kilimo katika Bonde la Kagera la mto Luiche katika Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa ajili ya uzalishaji chakula kwa wingi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Kilimo Kwanza.

Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza alisema hayo alipokuwa akizungumza na wakulima wa bonde hilo katika ziara ya siku saba mkoani Kigoma kukagua shughuli mbalimbali na miradi ya kilimo iliyo chini ya wizara yake.


Chiza alisema kuwa bonde hilo ni eneo muhimu kiuchumi nchini na yanayoweza kutumika kuzalisha kiasi kikubwa cha chakula kwa ajili ya matumizi ya ndani na ziada kwa ajili ya nchi jirani.


Alisema kuwa pamoja na umuhimu wa bonde hilo, halijatumika katika kuleta mapinduzi ya kilimo nchini. Alisema unahitajika uwekezaji mkubwa kulifanya bonde hilo kutumika kwa tija.


Naibu Waziri alisema kuwa atawapeleka wakulima wa bonde hilo ziara za kimafunzo katika mabonde mengine yanayofanana na hilo ili kupata uelewa wa kulifanya kuwa kichocheo cha uchumi.


Awali uongozi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji ulisema kuwa kwa miaka miwili mfululizo wamekuwa wakiomba kupatiwa Sh milioni 667 kwa ajili ya uendelezaji wa bonde na kufanya upembuzi yakinifu wa kina lakini bila mafanikio.


Katika risala kwa Naibu Waziri iliyosomwa na Mtendaji wa Kata ya Kagera, Hawa Kasongo uongozi huo wa manispaa ya Kigoma Ujiji ulisema kuwa mwaka 2002 walipatiwa Sh milioni 79 kati ya Sh milioni 200 walizoomba.


Alisema fedha hizo zilifanikisha upimaji na uchoraji wa michoro ya kihandisi pekee na kwamba hadi sasa hakuna shughuli nyingine iliyofanyika.


Bonde hilo lenye ukubwa wa hekta 5,500 na wakulima zaidi ya 5,000, baadhi ya wakulima wamelielezea kwamba kitendo cha serikali kushindwa kuliendeleza wanapata hasara kubwa kutokana na maji kujaa kwenye mashamba yao mara kwa mara.

No comments: