Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Tuesday, October 4, 2011

Precision Air yapongezwa kuruka tena Kigoma

MBUNGE wa Kasulu Mjini, Moses Machali amelipongeza Shirika la Ndege la Precision Air kwa kurejesha safari zake mkoani Kigoma baada ya kukaa kwa muda mrefu bila usafiri wa anga wenye uhakika.

Amesema kwa kuanza tena kwa safari hizo baada ya miezi kadhaa ya kukosa huduma hiyo, itaufanya usafiri wa abiria kuingia na kutoka Kigoma kuwa wa kuaminika na wa kutegemewa zaidi.


Akizungumza kwa simu jana, Machali anayetokana na chama cha NCCR-Mageuzi, alisema “kwanza nichukue fursa hii kuwapongeza Precision Air kwa uamuzi wao wa kurejesha safari hizi, maana tangu ATCL wajitoe safari za kuja na kutoka huku usafiri ulikuwa wa shida sana.”


“Hivi sasa usafiri wa shirika hili inatusaidia sisi wabunge, maofisa wa Serikali, wafanyabiashara na hata wananchi wa kawaida kutekeleza majukumu yetu kwa uhakika na kwa ufanisi zaidi. Muda ni mali,” alisisitiza.


Alisema kabla ya Precision Air kuingia katika soko la Kigoma, gharama za usafiri zilikuwa za juu mno, tofauti na sasa ambapo gharama zimepungua na kwa kiasi kikubwa imepunguza kero kwa mwananchi.


“Lakini tunashukuru kwa ushindani ulioletwa na Precision Air maana sasa tunaweza kwenda kwa nauli takribani laki tatu na ushee tu kwa kwenda na kurudi Dar es Salaam, ambayo ni gharama nafuu sana,” alisema Mbunge huyo wa Kasulu Mjini.


Meneja Mauzo wa Precision Air mkoani Kigoma, Abdallah Kijangwa alisema chaguo la Kigoma kuongezwa katika safari za mtandao wa shirika hilo haikuja kwa bahati mbaya.


“Kwenye utafiti wa awali wa masoko tuliofanya kabla ya kuanza safari za kuja huku, tuliona kwamba kuna mahitaji ya watu wengi sana kupata huduma ya usafiri wa ndege wa kuingia na kutoka mkoani hapa. Bila shaka Precision Air tumeonesha nia ya dhati kwa kutoa huduma hiyo,” alisema Kijangwa.


“Kwa sasa tuna safari jumla ya mara tatu kwa wiki kutokea Dar es Salaam kuja Kigoma, ambayo ni kwa siku ya Jumatatu, Jumatano na Ijumaa kwa ndege ya saa 12 asubuhi inayopitia Mwanza na kurejea kutoka Kigoma mchana wa siku hiyo hiyo. Muda si mrefu tutaongeza idadi ya safari zetu mkoani humo.”

No comments: