Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Thursday, October 13, 2011

Mikoa sita kuunganishwa Gridi ya Taifa na Kigoma ikiwemo

RAIS Jakaya Kikwete amepokea ripoti kutoka kampuni mbili za kimataifa kuhusu Mpango Kabambe wa mradi mkubwa wa umeme utakaounganisha kwenye Gridi ya Taifa mikoa sita ambayo kwa sasa haiko kwenye gridi hiyo.

Rais Kikwete alipokea ripoti hiyo kutoka kampuni za China National Machinery & Equipment Import & Export Corporation (CMEC) ya China na Siemens ya Ujerumani ambazo kwa pamoja zinatarajia kujenga kituo kikubwa cha kuzalisha umeme kutokana na gesi katika eneo la Mnazi Bay mjini Mtwara na pia kujenga njia ya kusafirisha umeme ya kilometa 1,100 kutoka Mtwara hadi Singida.


Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu jana, mradi huo mkubwa wa umeme wa megawati 300 utakaogharimu karibu Dola za Marekani milioni 684 na utakaozalisha umeme wa moja kwa moja na wenye nguvu kubwa ya kilovoti 300 (HVDC) utagharimiwa kwa pamoja na mkopo kutoka Benki ya Exim ya China na Serikali ya Tanzania.


Umeme kutokana na mradi huo utaunganishwa kwenye gridi ya taifa na kutoka Singida hatimaye utavutwa kupelekwa katika mikoa ya Kaskazini Magharibi mwa Tanzania ya Kagera, Kigoma na Rukwa ambako pia utaongeza upatikanaji wa umeme katika machimbo ya madini yaliyoko katika mikoa hiyo.


Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mbali na mikoa hiyo mitatu, pia mikoa ya Lindi na Mtwara ambayo nayo haiko katika Gridi ya Taifa nayo itaunganishwa katika Gridi hiyo kupitia umeme huo.


Kuunganishwa kwa mikoa hiyo sita katika Gridi ya Taifa kupitia umeme wa mradi huo pamoja na Mkoa wa Ruvuma ambao utaunganishwa katika Gridi hiyo kwa mradi unaogharimiwa na Serikali ya Sweden, kutakamilisha mpango wa Serikali ya Awamu ya Nne kuunganisha mikoa yote ya Tanzania kwenye umeme wa Gridi ya Taifa.


Kwa sasa, Mkoa wa Kagera unahudumiwa na umeme kutoka Uganda, wakati mikoa ya Kigoma na Rukwa inahudumiwa na umeme wa mafuta ya dizeli. Mikoa ya Mtwara na Lindi inapata umeme wake kutoka Kampuni ya Wentworth ambao haujaunganishwa kwenye gridi ya taifa.


Kuunganisha mikoa yote ya Tanzania kwenye Gridi ya Taifa ilikuwa moja ya ahadi kubwa zilizotolewa na Serikali ya Rais Kikwete wakati anaingia maradakani na kwa kuuunganisha mikoa hiyo sita kwenye gridi hiyo, Serikali hiyo itakuwa imetimimiza ahadi hiyo.


Akipokea ripoti hiyo, Rais Kikwete alizishukuru Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa juhudi zao zilizofanikisha makubaliano ya kujengwa kwa mradi huo mkubwa wa umeme utakaochangia kuongeza wingi wa umeme nchini katika kipindi ambacho kwa miezi kadhaa Tanzania imekabiliwa na mgawo wa umeme kutokana na ukame uliokausha maji kwenye mabwawa makubwa ya uzalishaji umeme nchini.


Rais Kikwete pia aliitaka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Benki ya Exim ya China kuhakikisha fedha za kutekeleza mradi huo zinapatikana haraka iwezekanavyo na pia ameitaka Tanesco na kampuni ya CMEC na Siemens baada ya kupatikana kwa fedha kuanza ujenzi wa mradi huo kwa kasi na kuukamilisha katika muda na ubora unaotarajiwa.

1 comment:

Anonymous said...

Kila la kheri,kwa mradi mkubwa wa umeme ambao utawasidia wananchi wa mikoa ambayo ilikua haina umeme wa kutosha,hayo ndo maisha bora sasa yatakayo mkomboa mwananchi wa hali ya chini.