Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Tuesday, October 4, 2011

Kituo Kikuu cha Mabasi Kigoma kujengwa

UJENZI wa Kituo Kikuu cha kisasa cha mabasi yaendayo nje ya Mkoa wa Kigoma kinatarajia kuanza mapema Novemba mwaka huu baada ya uongozi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji kusaini mkataba na kampuni ya ujenzi itakayojenga mradi huo.

Akizungumza katika kikao cha wadau wa maendeleo mjini Kigoma Mkuu wa Wilaya ya Kigoma,

John Mongela alisema kuwa kwa mkataba uliofikiwa mkandarasi wa ujenzi anatakiwa kuwa eneo la ujenzi wa mradi kuanzia Novemba 3, mwaka huu.

Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa stendi hiyo inayotarajia kujengwa katika eneo la Masanga mjini hapa inatarajia kugharimu kiasi cha Sh bilioni 2.5 ikiwa ni mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia unatarajia kubadilisha kwa kiasi kikubwa mandhari ya mji wa Kigoma Ujiji.


Sambamba na mradi huo alisema kuwa utaenda sambamba na miradi mingi ambayo nayo inafadhiliwa na Benki ya Dunia ambayo ameitaja kuwa ni pamoja na mradi wa ujenzi wa stendi ya daladala Kasingirima Ujiji itakayogharimu Sh bilioni 1.2 na stendi ya mabasi mjini Kigoma itakayogharimu Sh milioni 420.


Mongela alisema kuwa katika mpango huo pia Benki ya Dunia inatarajia kutoa kiasi cha Sh bilioni 7.4 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za kiwango cha lami katika mitaa mbalimbali ya Manispaa ya Kigoma na kwamba utekelezaji wa miradi hiyo utaanza katika kipindi kifupi kijacho.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Lewis Kalinjuna alisema kuwa pamoja na miradi hiyo inayofadhiliwa na Benki ya Dunia, Manispaa yake inatarajia kutumia kiasi cha Sh bilioni 14 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.


Katika fedha hizo, Kalinjuna alisema kuwa Manispaa hiyo inatarajia kutumia kiasi cha Sh milioni 300 ambayo ni maombi maalumu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba sita za watumishi wake, Sh milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari ya kidato cha tano na sita, Kata ya Kibirizi na maombi maalumu kwa ajili ya uendelezaji wa Hospitali Teule ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.


 

No comments: