WAKATI kampeni za uchaguzi mdogo Jimbo la Igunga zikishika kasi, CCM kimeamua kuwaongeza vigogo wawili wa ngazi za juu ili kuongeza mashambulizi dhidi ya wapinzani wao.Vyama vinavyoonekana kutoa upinzani mkali kwa CCM ni Chadema, ambacho kimemsimamisha Joseph Kashindye na CUF, kilichomsimamisha Leonard Mahoma.
Habari za uhakika kutoka ndani ya CCM, zilieza kuwa Katibu mkuu wake, Wilson Mukama na Mbunge wa Bumbuli, January Makamba, walitarajiwa kuwasili Igunga jana tayari kuungana na makada wengine kwenye kampeni hizo.
CCM wanaamini ushiriki wa viongozi hao akiwamo Makamba, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini na wengine ambao tayari wamepiga kambi Igunga, utasaidia kubadili upepo wa kisiasa jimboni hapa.
Habari kutoka vyanzo huru ndani ya CCM, vimedokeza kuwa hivi sasa kimeamua kutumia silaha zake nzito (makada mashuhuri) kuhakikisha kuwa jimbo hilo lililokuwa likishikiliwa na Rostam Aziz kabla hajajiuzulu, haliangukii upinzani.
Katibu wa Uchumi na Fedha, Mwigulu Nchemba, ambaye ndiye mratibu wa kampeni za CCM, jana alithibitisha ujio wa Mukama na Makamba akisema hiyo ni sehemu ya mipango yao.
“Wanakuja kuungana na makada wengine na wanaCCM ambao wako hapa (Igunga), kuhakikisha CCM kinaibuka na ushindi na kwa kweli kampeni zetu ni za kisayansi ambazo tayari zimetuhakikishia ushindi,” alisema Nchemba.
Makada wengine ambao wapo Igunga, ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uratibu na Uhusiano), Steven Wassira na Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi, John Komba, ambaye pia ni kiongozi wa Kikundi cha Sanaa CCM (TOT).
Alisema Dk Dalaly Kafumu ambaye ni mgombea wa CCM, hana sababu ya kutorithi mikoba ya Rostam kwa sababu tayari CCM kina mtaji wa zaidi ya wapiga kura 30,000.
Wakati CCM kikiwaita vigogo hao, Chadema nao wamemwita Naibu katibu mkuu wake na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kuongeza nguvu kampeni zinazoongozwa na Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa.
Habari za uhakika zilisema, Zitto anatarajiwa kuwasili hapa mwishoni mwa wiki hii kuongeza mashambulizi dhidi ya CCM na CUF, ambavyo ndivyo vyama vinavyoonekana kuwa na ushindani mkubwa.
Zitto alithibitisha kuwa njiani kuja Igunga na kuongeza kuwa, kampeni za chama hicho zitakuwa ni kali na zilizopangwa kikamilifu zikihusisha wabunge karibu wote wanaotokana na chama hicho.
No comments:
Post a Comment