Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Sunday, September 25, 2011

Watoto wafukiwa na kifusi, wafa Kigoma

WATOTO wawili wa familia moja ambao ni wanafunzi katika Shule ya Msingi Buronge, Manispaa ya Kigoma Ujiji wamekufa baada ya kufukiwa na kifusi cha mchanga wakati wakichimba mchanga kwa ajili ya kuuza na watoto wengine wawili wamejeruhiwa katika tukio
hilo.

Ofisa wa tarafa ya Kigoma Kaskazini, Mikidadi Daudi alisema kuwa watoto hao walikumbwa na tukio hilo juzi jioni majira ya saa moja na nusu katika machimbo hayo yasiyo ya rasmi kwa ajili ya kuchimba mchanga karibu na Shule ya Sekondari Buronge, Gungu mjini Kigoma.


Mikidadi aliwataja watoto hao kuwa ni Mussa Ibrahim mwenye umri wa miaka 16 na Yussuf Ismail (16) ambao wote ni wanafunzi wa darasa la sita katika shule hiyo ya msingi ya Buronge wakiwa pia wakazi wa kata ya Gungu, manispaa ya Kigoma Ujiji.


Aidha Ofisa Tarafa huyo alisema kuwa katika tukio hilo watoto wengine wawili ambao aliwataja majina kuwa ni Kayonko Jonas na Kassim Luhonyva walinusurika kifo baada ya kufanikiwa kujiokoa kutoka katika kifusi hicho.


Kamanda wa Polisi mkoa Kigoma, Fraiser Kashai alithibitisha kutokea kwa tukio na kusema kuwa hakuna mtu aliyekamatwa akihusika na tukio hilo kwani watoto hao walikuwa wakifanya shughuli hiyo wenyewe.


Machimbo hayo kwa muda mrefu yalikuwa yamezuia kwa ajili ya uchimbaji wa mchanga kutokana na athari za mazingira, lakini watu mbalimbali wamekuwa wakiendelea kuchimba mchanga kwa wizi na mara nyingi kazi hiyo hufanywa jioni baada ya saa za kazi.


Katika tukio jingine, Kamanda Kashai alisema kuwa mtoto mdogo mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu, John Chada amekufa baada ya kuangukiwa na mama yake mzazi kufuatia ugomvi wa kifamilia kati ya baba yake mzazi, mama yake na mke mwenza wa mama yake.


Alisema kuwa tukio hilo lilitokea mapema juzi asubuhi katika kijiji cha Murufiti mjini Kasulu na polisi inamshikilia baba mzazi wa mtoto huyo anayejulikana kwa jina la Chada Aliseni kwa mahojiano zaidi.

No comments: