Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Saturday, September 10, 2011

Wakemewa kuanika samaki, dagaa chini

MTINDO wa kuanika chini dagaa na samaki wanaovuliwa katika Ziwa Tanganyika mkoani hapa umetajwa kuchangia kushusha ubora wa bidhaa hiyo.

Mwenyekiti wa Shirika lisilo la kiserikali la Utawala Bora na Maendeleo (Uboma) la mjini hapa, Msafiri Wamalwa alisema hayo wakati wa uzinduzi wa mradi wa miezi mitatu kwa wadau wa uvuvi na viongozi wa kata za Kibirizi na Katonga katika manispaa ya Kigoma Ujiji . 


Mradi huo unalenga kufuatilia uwajibikaji wa wananchi na viongozi katika utekelezaji wa misingi ya utawala bora.

Wamalwa alisema kuwa kufanyika kwa jambo hilo ni ishara tosha ya kutotekelezwa kwa misingi ya utawala bora kwa viongozi na watendaji waandamizi wa serikali wakiwemo maofisa uvuvi na wataalamu wa afya kutokana na kushindwa kusimamia uanikaji wa kitaalamu.

Alisema kuwa katika utafiti mdogo ambao asasi yake imeufanya, imegundua kuwa wananchi wengi hawafahamu wajibu na majukumu yao katika suala zima la utekelezaji wa misingi ya utawala bora.

Ofisa Uvuvi katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, Sijaona Ngoroma alikiri kuwepo kwa udhaifu katika usimamizi wa sheria za uhifadhi rasilimali za uvuvi kutokana na wavuvi kuanika chini dagaa na samaki huku wakifahamu kufanya hivyo ni kosa.

Hata hivyo Ngoroma alisema kuwa mkakati wa idara za uvuvi katika halmashauri hizo ni kuhakikisha utaratibu wa kuhifadhi rasilimali za uvuvi kitaalamu unaoelekezwa kuwanusuru samaki na dagaa kukosa ubora.

No comments: