Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Saturday, September 10, 2011

Kigoma wakataa bei mpya ya maji

WATUMIAJI wa huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka katika Manispaa ya Kigoma Ujiji (KUWASA) wamekataa pendekezo lililotolewa na uongozi wa mamlaka hiyo la kutaka kupandisha bei ya maji kwa wateja wake kwa asilimia 400.

Katika kuonesha kwamba pendekezo hilo halijazingatia hali halisi ya utoaji huduma na maisha halisi ya mwananchi wa manispaa hiyo, Baraza la Watumiaji wa Huduma zinazodhibitiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (EWURA) na Baraza la Ushauri la Serikali yameungana na watumiaji hao katika kupinga pendekezo hilo.

Mapendekezo hayo ya KUWASA yalikataliwa katika kikao cha wadau kilichoitishwa na EWURA kilichofanyika katika ukumbi wa Kibo Peak ambapo wadau hao wamesema, hata kufanyika kwa kikao hicho hakuna maana kutokana na KUWASA kupandisha bei ya maji kabla ya kupata maoni ya watumiaji wake kama ilivyo taratibu.

Salum Mussa, mkazi wa Mwanga mjini Kigoma alisema kuwa maombi ya KUWASA kutaka kupandisha bei ya maji kutoka kiasi cha Sh 7,500 kinachotozwa sasa na kufikia Sh 31,000 kwa mwezi hakijazingatia uwiano katika upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi.

Awali, kabla ya kupitishwa kwa bei hiyo, Salum aliitaka EWURA kuichukulia hatua za kinidhamu kwa KUWASA kwa kupandisha bei ya maji kuanzia mwezi Machi mwaka huu kutoka wastani wa Sh 7,500 na kiwango cha chini kinachotozwa sasa kwa familia badala ya mita katika nyumba moja ni Sh 15,000.

Naye Lydia Ndika mkazi wa NORAD mjini Kigoma aliongeza kuwa KUWASA haina budi kuwaomba radhi wakazi wa mjini Kigoma kwa kitendo chake cha kupandisha bei ya maji bila kupata maoni ya watumiaji wake, lakini pia irudishe fedha ambazo imekuwa ikichukua katika uongezaji huo wa bei hadi hapo bei mpya itakapotangazwa na EWURA.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Baraza la Ushauri la watumiaji wa huduma zinazodhibitiwa na EWURA, Saidi Ahmed alisema kuwa bei zinazopendekezwa na mamlaka ya maji Kigoma Ujiji ni za kiwango cha juu sana ikilinganishwa na mamlaka za mikoa jirani kama Mwanza, Musoma na Bukoba ambazo pia vyanzo vyake pia ni kutoka ziwani kama Kigoma zikiwa katika daraja moja la utoaji huduma.

Ahmed ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa baraza hilo alisema kuwa matatizo mengi ya KUWASA hayatokani na bei zinazotozwa sasa isipokuwa zipo sababu dhahiri za matatizo ya kiutendaji ambayo yameleta ufanisi mdogo katika mfumo mzima wa mamlaka.

Akichangia, Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Serikali, Mhandisi Elizabeth Kingu alisema kuwa pamoja na sababu nyingine za kuongezeka kwa bei za vitu mbalimbali na kupanda kwa uchumi lakini maombi ya KUWASA kutaka kuongeza bei ya maji na huduma mbalimbali zinazotolewa naye hazijazingatia hali halisi ya mapato na matumizi ya mamlaka huku kukiona kukiwa na mapungufu makubwa ya kiutendaji.

Awali Mkurugenzi wa KUWASA, Simon Rubuga alito pendekezo la kupandishwaa kwa huduma mbalimbali zinazotolewa na mamlaka kwa asilimia 400 ili kukidhi mahitaji yake ya kiuendeshaji na mpango wa kuboresha huduma.

Katika hilo Rubuga aliomba mamlaka hiyo iruhusiwe kuongeza bili za maji kutoka wastani wa Sh 5,200 kwa bei za majumbani na kufikia Sh 31,000 kwa mwezi ambayo ni sawa la ongezeko la Sh 1,600 kwa mita moja ya ujazo kutoka mita 300.

Aidha katika maombi hayo ametaka kuongeza kwa bei kwa taasisi kutoka sh 450 kwa mita moja ya ujazo na kufikia Sh 2,400 huku viwanda na biashara vikitoka wastani wa Sh 600 kwa mita moja ya ujazo na kufikia Sh 2,600.

Kutokana na hilo, EWURA ambayo iliwakilishwa na Mkurugenzi wa Idara ya MajiSafi na Majitaka ilisema kuwa maombi hayo yatapelekwa katika bodi ya EWURA ambayo ndiyo itakayotoa majibu ya mwisho kuhusu viwango vipya vya nauli katika mchakato utakaochukua siku 180 ili kupatiwa majibu.


No comments: