Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Thursday, September 29, 2011

Viongozi Kigoma Ujiji lawamani kwa uchafu

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kigoma Ujiji inakabiliwa na uchafu unaodaiwa kuwa chanzo ni uongozi kutokana na kutokuwa na mpango kabambe katika kuuweka mji kwenye hali ya usafi. 



Mratibu wa Mradi wa uwiano wa maendeleo ya Bonde la Ziwa Tanganyika, Hawa Msham alisema hayo katika mkutano wa siku mbili wa kikosi kazi maalumu kilichopewa kazi ya kuandaa mpango na bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kuiwekea manispaa hiyo katika hali ya usafi.


Alisema kuwa katika kusimamia usafi wa manispaa yake, uongozi wa manispaa ya Kigoma Ujiji chini ya Idara ya Afya umekuwa ukifanya kazi zake kwa mazoea hali ambayo imetajwa kuwa haiwezi kukabili kuzagaa uchafu katika maeneo mbalimbali.


Kikosi kazi hicho kilikuwa kikipewa uzoefu na Ofisa Afya wa Manispaa ya Mji wa Mpanda, Pascal Kweha jinsi ya kuandaa mpango shirikishi jamii katika kuuweka mji safi.


Akizungumza katika mkutano huo, Kweha alisema kuwa Manispaa ya Mji wa Mpanda imefanikiwa kukabili uchafu kutokana na mipango mbalimbali waliyoiweka ambayo wananchi ambao ndiyo wazalishaji taka wakubwa ni wadau na wanachangia gharama za kudhibiti taka hizo.


Aliwaambia wajumbe hao wa kikosi hicho kuwa wananchi hawana tatizo kama watashirikishwa tangu mwanzo katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ili mradi mipango hiyo imeanzia kwao badala ya viongozi kukaa kwenye chumba na kupanga mambo yao bila kuwepo kwa ushirikishwaji wa jamii.


Awali akitoa taarifa ya hali ya taka za mji huo, Ofisa Afya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Ernest Nkonyozi alisema kuwa wakazi na masoko ya mji huo yanazalisha tani 107 za taka kwa siku lakini uwezo wa manispaa katika kuzoa taka hizo ni tani 41 kwa siku.


Alisema kuwa kwa kiasi kikubwa inasababishwa na uwepo wa rasilimali kidogo za kufanyia usafi ikiwemo tatizo la bajeti ndogo ya mafuta na magari na hivyo kufanya kiasi kikubwa cha taka kinachozalishwa kushindwa kuondolewa.

No comments: