Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Thursday, September 29, 2011

Mtaalamu aeleza madhara ya kutotunza misitu

MTAALAMU wa misitu katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) mkoani Morogoro, Profesa Emanuel Luoga ametahadharisha kuwa kushindwa kutekelezwa sasa kwa mpango wa usimamizi na matumizi endelevu ya misitu nchini, kutakuwa na athari kubwa siku za baadaye.

Profesa Luoga alisema hayo wakati akitoa mada katika mafunzo ya siku tatu kwa kamati za mazingira za vijiji sita vilivyopo kwenye mradi wa utunzaji mazingira wa Masito Ugalla unaosimamiwa na Taasisi ya Jane Goodall.

Alisema katika siku za hivi karibuni kumekuwa na mahitaji makubwa ya matumizi ya rasilimali za misitu na hasa inatokana na kuongezeka kwa idadi ya watu, lakini alibainisha kuwa matumizi hayo ya misitu yanapaswa kuwekwa katika mpango ya utekelezaji na kuona namna ya kuendelea kulinda ili idumu muda mrefu.

Aliwaambia washiriki wa mafunzo hayo kwamba mabadiliko ya tabianchi yanayotokea duniani hivi sasa chimbuko lake linatokana na matumizi yasiyo endelevu ya misitu na nishati yaliyofanywa miaka mingi iliyopita.

Hivyo, aliwaambia washiriki hao kuwa wanao wajibu mkubwa wa kuhakikisha maeneo wanaoishi na kufanyia shughuli zao, hayana budi kutumika katika namna isiyoathiri mazingira na kuwaletea madhara baadaye.

Kwa upande wake, Ofisa Maendeleo ya Jamii ya Mradi wa Masito Ugalla, Naomi Lumenyera alisema kuendelea kuathirika kwa mzingira katika maeneo mbalimbali nchini kunatokana na wananchi kutoona umuhimu wa kuhifadhi mazingira na zaidi kujali maslahi yao.

Lumenyera alisema licha ya kupata elimu ya utunzaji mazingira, inashangaza kuona hao hao waliopata elimu ndiyo wanaoingia ndani ya msitu katikati na kuanzisha shughuli za kibindamu ikiwemo kilimo na makazi.

Alisema mradi unatekeleza jukumu lake la kuwapatia elimu viongozi na wananchi wa vijiji mbalimbali mkoani Kigoma, lengo likiwa kuwafanya watambue madhara ya matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali za misitu.

 

No comments: