Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Thursday, September 29, 2011

Mkurugenzi Misitu awatangazia vita wanasiasa Kigoma

MKURUGENZI wa Idara ya Misitu na Nyuki, Dk Felician Kilahama amesema kuwa yuko tayari kupoteza wadhifa huo kwa kupambana na viongozi wa kisiasa wanaohamasisha wananchi kufanya shughuli mbalimbali katika hifadhi za misitu nchini.

Akizungumza katika mkutano wa majumuisho ya ziara yake ya siku tatu mkoani Kigoma, Dk Kilahama alisema kuwa viongozi wa kisiasa wamekuwa chanzo kikuu cha migogoro ya ardhi na kuchangia uvunaji wa rasilimali za misitu usiozingatia sheria.


Alisema kwa muda mrefu hata ofisini kwake amekuwa akipata barua na malalamiko yanayohusu viongozi wa kisiasa kutaka kuruhusu kufanya shughuli kwenye hifadhi au kuvuna rasilimali za misitu bila kufuata sheria.


Alisisitiza kuwa hatakubaliana na jambo hilo.


Alisema atajitahidi kwa nguvu zake kupambana na uharibifu wa mazingira na uvunaji rasilimali za misitu usiozingatia sheria na hatakubali kumuonea haya kiongozi anayehamasisha wananchi kuingia kwenye hifadhi za misitu kuvuna, kulima au kufanya shughuli yoyote.


“Kama nitapoteza kazi yangu kwa kusimamia jambo hili, niko tayari,” alisema.


Akizungumzia hali ya uharibifu wa mazingira nchini, alisema kuwa umekuwa mkubwa kuliko wakati wowote katika kipindi hiki cha miaka 50 ya uhuru.


Alisema asipotokea mtu wa kujitoa mhanga kusimamia matumizi endelevu ya misitu na hifadhi za msitu, hali itakuwa mbaya siku za baadaye na kusababisha matatizo makubwa kwa nchi.


"Ukame na matatizo yanayotokea katika nchi mbalimbali duniani chanzo chake ni kama ambavyo inafanyika sasa nchini, tusipokuwa wakali sasa na kuruhusu misitu yetu kuharibiwa

ni wazi tutakuja kulia siku za baadaye kama ambavyo mkoa wa Shinyanga unalia sasa," alisisitiza Dk.Kilahama.

Baadhi ya wadau waliohudhuria mkutano huo wa majumuisho wameishutumu serikali kuchangia uharibifu wa misitu wakidai Idara ya Misitu haitengewi fedha za kutosha katika bajeti ya kila mwaka.


Ofisa Mazingira wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Leonard Nzilaikunde alisema kuwa maofisa misitu na mazingira katika halmashauri wamekuwa wakifanya kazi muda mwingi wakiwa ofisini badala ya msituni kutokana na uhaba wa rasilimali ikiwemo mafuta na posho.


Kwa mujibu wa Nzilailunde, karibu misitu yote nchini haina walinzi na kwamba serikali iliwaondoa ili kubana matumizi. “Lakini kwa sasa hali ni mbaya zaidi kwa kile kinachotokea kuliko mawazo ya baadhi ya viongozi katika kutekeleza ubanaji huo wa matumizi ya serikali,” alisema.

No comments: