Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Monday, September 26, 2011

Simbakalia ajisifia uongozi wake Kigoma

ALIYEKUWA mkuu wa mkoa wa Kigoma, Joseph Simbakalia amesema anaondoka akiwa amefarijika kwa kuufanya mkoa huo kuwa wenye neema tofauti na alivyoukuta. 



Alisema baada ya wananchi kukata tamaa kwa muda mrefu kuwa mkoa huo umetengwa, sasa umeanza kufunguka na kuimarika kiuchumi.


Simbakalia ambaye amehamishiwa Mkoa wa Mtwara alisema hayo katika sherehe za kumuaga zilizofanyika mjini hapa.


Alitoa mwito wananchi wa mkoa huo kuitumia fursa hiyo kujiimarisha kiuchumi.


Alisema kuwa alifika mkoani humo akikuta watu wakiwa wamekata tamaa na kuitupia lawama serikali kwa kuutenga kiuchumi na kuacha watu wake wakiendelea kuwa masikini.


Hata hivyo alisema kwa kipindi cha miaka mitano aliyokaa mkoani Kigoma, aliweza kubadili hali hiyo na kuifanya Kigoma kuwa yenye neema na mafanikio.


Kwa mujibu wake, katika kipindi chake cha miaka mitano mkoani Kigoma miradi mikubwa ya kimaendeleo imetekelezwa ikiwemo ujenzi wa barabara za kiwango cha lami, ujenzi wa daraja la Malagarasi.


Pia alisema Kigoma umekuwa ukanda maalumu wa kiuchumi na kwamba kuanzia Novemba ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa mkoani humo utaanza.


Alibainisha kuwa mafanikio hayo yamepatikana kutokana na ushirikiano alioupata kutoka viongozi wenzake na watendaji wa sekta mbalimbali na kwamba bila ushirikiano huo mafanikio hayo yasingeweza kupatikana.


Alisema kuwa anaondoka mkoani Kigoma akiwa hana kinyongo wala chuki na mtu yeyote na

akatangaza kuwasamehe wanaohisi kuwa na chuki naye.

Awali Katibu Tawala msaidizi huduma za utawala, Anthony Jakonyango alisema Simbakalia

anaacha kumbukumbu kubwa.

No comments: