Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Saturday, September 10, 2011

DC aitaka Saccos itoe mikopo ya kilimo Kigoma

MKUU wa Wilaya ya Kigoma, John Mongella, amekitaka Chama cha Akiba na Mikopo Kigoma cha Jikomboe Saccos kutoa mikopo ya kilimo kwa wanachama wake ili kuunga mkono dhana ya Kilimo Kwanza na uamuzi wa serikali kuwa moja ya mikoa inayozalisha chakula kwa wingi.

Akifungua Mkutano Mkuu wa Jikomboe Saccos mwishoni mwa wiki, Mongella alieleza kuwa kilimo kwa sasa ni moja ya mambo ya kipaumbele ambayo serikali inayasimamia.


Mongella alisema wakati Jikomboe Saccos ikitoa mikopo, serikali itakuwa imeshaweka mazingira mazuri ya kuwapatia maeneo ya kilimo wanachama wa chama hicho huko Lugufu, Kigoma Vijijini ambako kwa sasa serikali imeamua kulifanya eneo hilo kuwa maalumu kwa kilimo.


Alisema chama hicho kinaweza kuchukua maeneo ya kilimo na kununua trekta kwa kazi hiyo ikawa kama moja ya vitega uchumi vyake na serikali ikaiwekea mazingira mazuri ya kufanikisha jambo hilo.


Alisema kwa sasa chama hicho kinao mtaji wa kutosha wa kufanya jambo inalotaka na kuupa uongozi changamoto ya kuona namna gani wanaweza kufanya mageuzi na kuifanya kuwa benki ya wananchi.


Akitoa taarifa ya hali ya utoaji mikopo, Ofisa Mikopo wa Jikomboe Saccos, Shingwa Hamisi alisema mikopo ya Sh bilioni 3.4 imetolewa kwa wanachama 760 na kumekuwa na marejesho yanayoridhisha.


Shingwa alisema mkopo huo kwa wanachama umewezekana kutokana na mkopo wa Sh bilioni 2.6 waliopata kutoka Benki ya CRDB na sasa chama hicho kinakusanya zaidi ya Sh milioni 150 kila mwezi marejesho na riba ya karibu Sh milioni 15.


Ofisa Mikopo huyo alisema sehemu kubwa ya mikopo ya wanachama ambao ni watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma imeelekezwa kwenye biashara, kilimo, ujenzi na mahitaji mengine ya kijamii, ikiwemo kugharamia matibabu na shughuli nyingine za kijamii.

No comments: