Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Sunday, September 18, 2011

ATCL kuruka tena Tabora, Kigoma

KAMPUNI ya Ndege Tanzania (ATCL), imesema iwapo mipango yao itakwenda vizuri, wanaweza kuanza safari za kila siku za kwenda mikoa ya Tabora na Kigoma mwishoni mwa wiki ijayo.

Akizungumza katika kipindi cha Jambo Tanzania cha TBC1 kuhusu miaka 50 ya Uhuru na uhai wa kampuni hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Paul Chizi alisema huduma
hiyo itarejea kutokana na kuwasili kwa ndege yake ya DASH 8-300 kutoka Afrika Kusini ilikopelekwa kwa matengenezo. 


“Ndege iliwasili Jumamosi iliyopita na mambo yakiwa mazuri, hadi Septemba 25 tutaanza safari za moja kwa moja kila siku katika mikoa ya Tabora na Kigoma,” alisema Chizi.

Alisema wanaangalia makosa yaliyojitokeza ili kuyarekebisha na kusonga mbele, kwa kujipanga upya kuhakikisha wanakabiliana na ushindani uliopo na ili wasiyumbe tena kama
ilivyotokea.

“Katika ushindani tunakwenda na mbinu mpya, tunawapa wafanyakazi mafunzo ya mara kwa mara ya namna ya kukabiliana na changamoto zilizopo na ushindani wa biashara, tunatakiwa
kuwafurahisha wateja wetu la sivyo hatuwezi kwenda mbele,” alisema.

“Tunataka Serikali ikishatupa mtaji basi tujitegemee, tulipe mishahara wenyewe na tunaamini Watanzania wanaipenda ATCL yao na tunawaomba watupe ushirikiano wa karibu ili tuwape huduma bora,” alisema Kaimu Mkurugenzi wa kampuni hiyo ya umma.

Alisema wamejipanga kulimudu soko la ndani kwanza kabla ya kuangalia masoko ya nje, huku akiahidi kuwa baada ya miaka mitatu, ATCL itarudi katika hali yake ya kawaida.

Alisema kuna ndege nyingine ya DASH-8-300 ambayo wanatarajia kuifanyia matengenezo nchini. Katika mikakati yake, Chizi alisema tayari ATCL imeingia mkataba na Kampuni ya Jetlink (T) Ltd ili kupata ndege nyingine ambayo itatumika tu pale ndege ya kampuni hiyo inapokuwa na hitilafu.

No comments: