Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Friday, August 26, 2011

Zitto kujiuzulu ubunge


MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma, Kabwe Zitto amelieleza Bunge kuwa, endapo itabainika kwamba, mjumbe yeyote wa kamati hiyo alipewa rushwa katika suala la kuiongezea muda taasisi ya Serikali inayosimamia ubinafsishaji wa mashirika ya umma (CHC), si tu atajiuzulu uenyekiti wa kamati hiyo lakini pia atajiuzulu ubunge.

Zitto ametoa ahadi hiyo leo bungeni mjini Dodoma wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitia vifungu vya bajeti ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2011/2012.

Amemtaka Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo naye aliahidi Bunge kuwa ikibainika viongozi wa Serikali walipewa rushwa ya shilingi milioni 60 ili CHC waruhusiwe kufanya kazi hiyo moja kwa moja atajiuzulu.

Mkulo hajatoa ahadi ya kujiuzulu, amesema kwanza uchunguzi ufanyike ndipo lije suala la kujiuzulu au la.

Kwa mujibu wa Zitto, katika hadidu za rejea alizopewa Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) za kuchunguza tuhuma za ubadhirifu CHC, suala la rushwa hiyo halipo.

Mbunge huyo alimtaka Mkulo aagize tuhuma hizo za rushwa ziingizwe kwenye hadidu za rejea alizopewa CAG, na pia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), aagize Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ichunguze tuhuma hizo kwa uwazi.

Mkulo amesema, suala hilo litafanyiwa kazi kwa mujibu wa taratibu za Serikali, na kwamba, Bunge litapewa taarifa.

Spika wa Bunge, Anne Makinda, amesema, amepata malalamiko ya wafanyakazi wa CHC lakini hakukuwa na tuhuma za rushwa inayosemwa.

Awali, wakati anajibu hoja za wabunge waliochangia bajeti ya Wizara hito, Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo amelieleza Bunge kuwa, Waziri Kivuli wa Wizara hiyo, Kabwe Zitto ni muongo na mzushi.

Waziri Mkulo amesema, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CHC, Mathusela Mbajo, hajafukuzwa kazi, kapewa likizo ili CAG amchunguze. Mkulo amewaeleza wabunge kuwa, hajaagiza kiongozi huyo wa CHC afukuzwe kazi ila tuhuma dhidi yake kuhusu ubadhirifu ni nzito.

Jana wakati anawasilisha hotuba ya Kambi ya Upinzani kuhusu bajeti ya Wizara ya Fedha, Zitto alisema, Mathusela amesimamishwa kazi kwa tuhuma zilizozaa majungu kutoka kwa wanaojiita wafanyakazi wa CHC.

“Kufuatia maagizo ya Waziri wa Fedha kwa Bodi ya Wakurugenzi wa CHC Mtanzania huyu kazimamishwa kazi na kwamba, CAG ameombwa kuchunguza majungu yale kutoka kwa mwanaojiita wafanyakazi wa shirika la CHC” alisema Zitto.

Kambi hiyo imepinga uamuzi wa Mkulo kwa maelezo kuwa, amekiuka Sheria namba 3 ya mwaka 1988 ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge na ilitaka maelezo ya Mkulo kwa nini ameamuru Kaimu Mkurugenzi wa CHA aende likizo wakati anafahamu kuwa suala hilo lipo mezani kwa Spika wa Bunge.

“Bunge hili linapaswa kusimama imara kuzuia kuingiliwa kwa mamlaka yake na tawi la utendaji. Mijadala ndani ya Bunge inalindwa na Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Tusipokuwa makini Bunge litaendelea kudharauliwa na hivyo kushindwa kufanya kazi yake ya kuwawakilisha wananchi, kutunga sheria na kuisimamia Serikali ipasavyo” alisema.

1 comment:

mruta julius said...

Ni nzuri kuonesha umakini na kuaminiana kwa watu anaofanya nao kazi lakini awe makini isiwe ni mtego, kwani shutuma za wabunge kuhongwa ili kupitisha baadhi ya hoja za serikali imeenea sana na ukweli upo(Kafulila dhidi ya Zambi).