Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Wednesday, August 24, 2011

TaCRI kuongeza uzalishaji bora wa kahawa


TAASISI ya Utafiti wa Kahawa (TaCRI) inakusudia kuongeza uzalishaji wa kahawa bora ya vikonyo kutoka tani 1,200 kwa mwaka hadi kufikia tani 11,500 ifikapo mwaka 2020.

Mkurugenzi Mtendaji wa TaCRI, Profesa James Terry alisema hayo juzi katika maadhimisho ya miaka 10 ya kuzaliwa kwa taasisi hiyo kwenye kituo cha Mwayaya tarafa ya Manyovu wilayani Kasulu.

Profesa Terry alisema kuwa mkakati huo wa kuongeza uzalishaji unatokana na mafanikio ya utafiti uliofanywa na taasisi yake.

Alisema kuwa Mkoa wa Kigoma una fursa za kuchangia mafanikio ya mkakati huo kutokana na kuwa na maeneo ya kutosha kwa ajili ya upanuzi wa mashamba lakini pia una nguvu kazi ya kutosha na rasilimali muhimu katika uzalishaji kama ardhi na hali nzuri ya hewa.

Mkurugenzi huyo wa TaCRI alisema kuongezeka kwa uzalishaji wa kahawa nchini, kutachangia kuongeza kipato cha wakulima wa zao hilo kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya zao hilo duniani kote baada ya kuongezeka kwa wanywaji maradufu.

Kwa upande wake Meneja wa TaCRI Mkoa wa Kigoma, Epimaki Tarimo alisema mkoa huo
kwa kutumia kituo cha utafiti cha Mwayaya umeweka mkakati wa kuzalisha miche milioni 20 ya kahawa ya vikonyo ifikapo mwaka 2020 mkakati ambao utawezesha mkoa huo kuzalisha miche milioni tatu kwa mwaka.

Kwa mujibu wa Tarimo, kahawa ya Kigoma imeendelea kuongoza kwa ubora na yenye muonjo unaopendwa na wanywaji katika soko la dunia na mkakati ni kuongeza maradufu uzalishaji wa kahawa hiyo.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Dahn Makanga kwa niaba ya Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza amezitaka halmashauri za wilaya nchini kuweka mkakati huo katika bajeti Mpango wa Maendeleo ya Kilimo wa Wilaya (DADPs).

No comments: