Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Wednesday, August 24, 2011

Wabunge- Bunge limedhalilishwa, Pinda kafedheheshwa


 
BUNGE limesema, Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo amelidhalilisha na pia amemdhalilisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa kumuamuru Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo arudi kazini.

Wabunge wamesema, taarifa ya uchunguzi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu tuhuma kwamba, Jairo alichangisha shilingi bilioni moja ili kuwezesha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ipitishwe bungeni ilistahili kupelekwa bungeni waijadili kabla Serikali kutoa uamuzi.

Wabunge leo wamejadili kauli ya Luhanjo kama jambo la dharura baada ya wabunge kukubali hoja ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto aliyoitoa asubuhi kabla ya kipindi maswali na majibu na kuifafanua baada ya Kamati ya Bunge ya Uongozi kukutana katika ukumbi wa Spika.

Spika wa Bunge, Anne Makinda aliongoza kikao hicho cha dharura wakati wa kipindi cha maswali na majibu.

Kabla ya kamati hiyo kukutana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema, kwa kutumia kifungu cha 51 cha Kanuni za Bunge alichotumia Zitto kuwasilisha hoja yake, inamtaka Mbunge aiwasilishe mapema kwa Spika wa Bunge ili atoe uamuzi.

Naibu Spika Spika wa Bunge, Job Ndugai, alimjibu Lukuvi kwamba, kabla ya kuanza kwa kikao cha leo, Zitto alipeleka taarifa fupi kwa Spika wa Bunge kuhusu hoja hiyo kwa hiyo utaratibu umefuatwa.

“Hoja hii nzito kweli…na ndiyo hoja iliyoungwa mkono” amesema Ndugai baada ya Zitto kuiwasilisha kwa mara ya kwanza kabla ya.

Zaidi ya robo tatu ya wabunge waliokuwa ukumbini wakiwemo kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameunga mkono hoja ya Zitto. Ndugai, amesema bungeni kuwa, hoja ya Zitto ni ya msingi kwa kuwa Bunge limedharauliwa.

“Kwa sababu Bunge ni mhimili, hatuwezi kudharauliwa kirahisi”amesema Ndugai na kusisitiza kwamba,Wabunge hawawezi kukaa kimya wakati Waziri Mkuu anadhalilishwa.

“Kama dharau inaweza ikatokea basi huko huko lakini sio ndani ya Bunge hili” amesema Ndugai baada ya wabunge kuijadili hoja ya Zitto na kusisitiza kwamba, kwa kuwa suala hilo lilianzia bungeni, taarifa ya CAG ingepelekwa kwanza kwenye mamlaka hiyo kabla ya uamuzi wa Serikali.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Zainab Vullu, wabunge wamepewa jukumu la kuisimamia na kuishauri Serikali kwa niaba ya wananchi hivyo kauli ya Luhanjo imewadhalilisha, na limepokwa mamlaka yake.

Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, amesema, suala hilo lina maslahi kwa Taifa, taarifa ya CAG ingepelekwa kwanza bungeni itendewe haki.

Sendeka amesema bungeni kuwa, Waziri Mkuu amefedheheshwa kwa kuwa Kiongozi huyo wa Shughuli za Serikali Bungeni alisema, kama angekuwa yeye angemchukilia hatua Jairo, na pia Bunge limedhalilishwa.

Kwa mujibu wa Sendeka, kauli ya Luhanjo imelilidhalilisha Bunge na imekiuka Sheria ya Kinga na Madaraka ya Bunge na ibara ya 100 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Mbunge huyo ametumia Kanuni 117 ya Bunge kuomba iundwe kamati teule ya Bunge kuchunguza jambo hilo ukiwemo utaratibu wa Jairo kukusanya fedha za kupitishia bajeti hasa ikizingatiwa kuwa, kila Waziri huwa na fungu la kugharamia bajeti kila idara zikiwemo fedha za kununulia mafuta.

Sendeka aliomba Bunge liunge mkono hoja yake ili kulinda hadhi ya Bunge, takribani wabunge wote walikubali isipokuwa mawaziri na manaibu mawaziri.

Wakati anatoa hoja hiyo, Zitto amesema, kwa kuwa jambo hilo lilianzia bungeni wakati Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo (CCM) alipolieleza Bunge kuwa ana barua ya Jairo kuzitaka idara katika Wizara za Nishati na Madini zichangie shilingi milioni 50 kila moja, wabunge walistahili kuijadili ripoti ya CAG kabla ya Serikali kufanya uamuzi.

Zitto amelieleza Bunge kuwa, kauli ya Luhanjo ni dharau kwa Waziri Mkuu, na imeingilia hadhi, kinga na madaraka ya Bunge kwa kuwa wabunge ndiyo wana mamlaka ya kuisimamia Serikali.

Zitto alipendekeza kwamba, shughuli na hoja zote za Serikali bungeni zisitishwe, kwanza wabunge waijadili taarifa za CAG kwa kuwa Bunge limepokwa nafasi yake.

Ndugai amewaeleza wabunge kuwa, Spika wa Bunge, Makinda, ataunda tume kuchunguza kudharauliwa kwa Bunge, na kukusanywa kwa fedha kwa ajili ya kupitishwa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2011/2012.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa Bunge, tume hiyo itapaswa kufanya kazi haraka ili taarifa yake ijadiliwe katika mkutano ujao wa Bunge.

Luhanjo jana alimuagiza Jairo arudi kazini leo aendelee na madaraka yake katika Wizara ya Nishati na Madini kwa kuwa tuhuma zilizotolewa dhidi yake hazikuthibitika.

Leo asubuhi, Jairo alikwenda ofisini kwake wizarani jijini Dar es Salaam, wafanyakazi wakampokea kwa shangwe na vigelegele huku wakiimba kwamba wana imani naye.

No comments: