Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Tuesday, August 23, 2011

Ulevi watia doa elimu Kigoma

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Nabuhima Wilaya ya Kibondo wakiwa darasani.

BABA wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kuwa ‘Timiza wajibu wako, inawezekana’.

Maneno hayo yalisemwa miaka mingi iliyopita, lakini yanapokumbushwa sasa ni dhahiri huonekana kama yaliyosemwa jana.Katika utumishi wa umma, maneno hayo ya Baba wa Taifa, yana maana kuwa kila aliyeingia huko, anapaswa atimize wajibu wake kwa kufanya kazi na kutimiza majukumu yanayomkabili.

Kushindwa kutimiza majukumu, ndiyo matokeo ya kuharibika kwa mambo mengi nchini mwetu, miongoni mwa hayo ni pamoja na kuwepo kwa usimamizi mbovu wa watendaji wa elimu katika halmashauri.

Hivi karibuni, nilifanya ziara katika shule za msingi na sekondari kwenye wilaya za Kasulu na Kibondo mkoani Kigoma, kuangalia suala la hali ya elimu na taaluma kwenye shule hizo. Pamoja na mambo mengi ikiwemno utoro uliokubuhu wa wanafunzi, lakini pia nilikutana na utoro wa walimu, ulevi wa kupindukia.

Mambo mengine ambayo kwa kutotimiza wajibu wao, yamewaondolea sifa ya ualimu walio kuwa nayo.Miaka mingi walimu walikuwa wakichukuliwa kama kioo cha jamii (role model) katika maeneo yao, ambapo kila mwanafunzi aliyekuwa akiulizwa wakati huo, unataka kufanya kazi gani baada ya kumaliza masomo yake, jibu lake linakuwa nataka kuwa mwalimu.

Ualimu ni mwito na kwa misingi hiyo mwalimu alifanya kazi yake kutoka ndani ya moyo, hasa kulingana na mazingira duni ya shule, nyumba za kuishi na hata miundombinu ya barabara kuingia na kutoka katika maeneo wanayoishi na kufanyia kazi.

Kwa hakika mwalimu alijituma na kutimiza wajibu wake kweli kweli na hata matokeo ya wanafunzi yalikuwa mazuri licha ya walimu hao kufanya kazi katika mazingira ambayo Mwenyezi Mungu ndiye anayejua ugumu wake.

Kutokana na hali hiyo Serikali na wadau mbalimbali na wahisani wa ndani na nje ya nchi wamejitahidi kwa hali na mali kuhakikisha kwamba wanaboresha mazingira ya kufundishia na kuishi walimu ili kupunguza adha zilizokuwepo.

Kuwapo Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Sekondari (MMES) ni moja ya malengo ya Serikali na wadau katika kuboresha hali ya elimu nchini.

Nikiwa katika ziara hiyo ya kielimu, nilipata bahati ya kuongea na Ofisa Elimu wa Shule ya Msingi katika Wilaya ya Kibondo, Bilungama Nyalinga, ambaye katika mazungumzo yetu alizungumzia suala la utovu wa nidhamu wa walimu.

Nyalinga anasema kuwa walimu wengi wa shule za msingi ni walevi wa kupindukia na watoro waliokubuhu, hali ambayo kwao ni mzigo inachangia kushusha taaluma.

Kutokana na hilo, Nyalinga anasema kuwa wamewachukulia hatua walimu 24 na kuwashitaki katika Tume ya Utumishi ya Walimu (TSD), kwa ajili ya kuwachukulia hatua za kinidhamu.

Pamoja na kufungua mashitaka hayo mwaka 2008, Nyalinga anasema kuwa ni kama TSD haipo, kwani hadi sasa mashitaka (mashauri) hayo hayafanyiwa kazi na walimu walioshitakiwa bado wanafanya kazi kama kawaida.

Bila kuchukuliwa hatua yoyote. Kwa kiasi kikubwa kitendo cha TSD kushindwa kuchukua hatua za kinidhamu kwa walimu, kinachochea vitendo vya utovu wa nidhamu kwa walimu wengine, kwa kuona wenzao walioshitakiwa mwanzo, hawakufanywa chochote.

Anasema kuwa utendaji kazi wa TSD ni mzigo mkubwa kwa halmashauri, kwani ndiyo mamlaka ya kisheria ya nidhamu na ambayo inapaswa
itoe adhabu au maelekezo kwa mwajiri (Halmashauri) hatua za kuchukua kwa mwalimu mkosaji.

Hata hivyo, sikubahatika kukutana na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu Wilaya ya Kibondo, kuelezea changamoto hiyo ambayo imetupiwa lawama kwao, kwa kile nilichoelezwa kwamba alikuwa nje ya wilaya kwa muda mrefu kwa shughuli za kikazi.

Lakini, nilipata nafasi ya kufanya mahojiano na Katibu wa Tume ya utumishi wa walimu Mkoa Kigoma, Yael Rushahu, ambaye alipinga madai ya maofisa Elimu wa Halmashauri, ambao wanaitupia lawama Tume yake kuhusu utovu wa nidhamu wa walimu.

Anaeleza kuwa wakuu wa shule, ndiyo wanaopaswa kuwa wa kwanza kutoa taarifa za utovu wa nidhamu za walimu wao, lakini hawafanyi hivyo na wanafanya hivyo ili kukwepa kutimiza wajibu wao.

Pamoja na hilo, anasema kuwa yupo Mratibu wa Elimu wa Kata, kamati za maendeleo za kata na wadau, ambao kwa pamoja wana majukumu makubwa katika kuangalia maendeleo ya sekta ya elimu katika maeneo hayo. Hivyo inaonesha wazi kuwa zipo taratibu na mamlaka za kisheria za kusimamia utendaji wa kila siku wa walimu na maendeleo ya shule, lakini viongozi hao hawatimizi wajibu wao.

Anasema kuwa zipo ofisi za ukaguzi katika halmashauri, ambazo zina mamlaka na madaraka ya kufanya ukaguzi na kutoa taarifa mamlaka zinazohusika kwa ajili ya kuchukua hatua.

Anasema kuwa wakati mwingine, maofisa elimu kwa kujitoa Kimasomaso, huwaletea mashitaka ya utoro, utovu wa nidhamu na ulevi wa kupindukia wa walimu ikiwa imepita muda mrefu tangu vitendo hivyo vilipofanyika.

“Mwalimu Mkuu anaona, Kamati ya Shule inaona, Mratibu Elimu Kata anaona na wakati mwingine hata Ofisa Elimu, wanakuwa wapi kuchukua hatua mapema dhidi ya vitendo hivyo hadi vinapopindukia ndiyo wanatoa taarifa” analalamika Rushau.

Kisheria, kwa muundo wa Tume ya Utumishi ya walimu, hawana mamlaka ya kuingilia utendaji wa halmashauri wala shule na kwamba jukumu lao ni kuletewa mashitaka, kufanya uchunguzi na hatimaye kuchukua hatua kwa matokeo ya uchunguzi walioufanya.

Katika baadhi ya mashitaka wanayoletewa, yapo ambayo kiuchunguzi, waliangalia na kuona kuwa ilikuwepo tofauti ya kimahusiano kati ya mfungua mashauri na mwalimu ; au mashitaka yaliyofunguliwa hayakuwa na nguvu kisheria ya adhabu, ambayo mwajiri anadhani mtumishi anastahili.

Tatizo liko hapo. Wakati mwingine ni mashitaka ya majungu tu ndiyo yanayofunguliwa, au mashitaka yanafunguliwa mtumishi akiwa amefanya vitendo hivyo miaka mingi. Pamoja na hayo, tume hiyo imekuwa ikifanya uchunguzi na kuchukua hatua muafaka, kulingana na makosa yaliyofunguliwa na mwajiri na hatimaye kutoa adhabu inayostahili.

Rushahu anasema mamlaka za ukaguzi za wilaya na mkoa, zinapaswa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika shule na kutoa maelekezo sahihi kwa mamlaka zinazohusika ili kuchukua hatua.

Azungumza na gazeti hili, Mkaguzi Mkuu wa Shule Kanda ya Ziwa Magharibi, Deodatus Lyapambile, anasema mamlaka za ukaguzi, ikiwemo yao inafanya ukaguzi wake kila siku na kutoa mapendekezo ya nini cha kufanywa.

Hata suala la upungufu wa walimu na utoro wa walimu na mambo mengine, mamlaka yake imeshafanya ukaguzi na kutoa taarifa na mapendekezo ya hatua za kuchukua kukabiliana na hilo.

Lakini, anasema kuwa taarifa yao ya ukaguzi ni siri na kamwe hawapaswi kuitoa nje, zaidi ya mamlaka yao ya kuripoti na kwa wadau wanaohusika. Lyapambile anasema yapo mambo ambayo wametoa ushauri nayakafanyiwa kazi, ikiwemo upungufu mkubwa wa walimu katika maeneo ya pembezoni na jinsi unavyochangia kushusha taaluma.

Anasema kuwa hata suala la kuongezwa kwa posho ya walimu katika maeneo yenye mazingira magumu ni wazo ambalo linatokana na ukaguzi, walioufanya na kubaini kuwa kuwepo kwa posho hiyo kunaweza kusaidia walimu kwenda maeneo hayo.

Anasema suala hilo halipaswi kuachiwa mtu mmoja na kwamba uwajibikaji wa pamoja ( collective responsibility), ndiyo unatakiwa na kila mmoja anatakiwa kutimiza wajibu wake.

No comments: