Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Tuesday, August 23, 2011

Kigoma washindwa kutumia bilioni 2.7/-


HALMASHAURI ya Wilaya ya Kigoma imeelezwa kushindwa kutumia kiasi cha Sh bilioni 2.7 zikiwa ni fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi kwa mwaka wa fedha wa 2009/2010.

Akitoa majibu ya hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali za Mitaa, juu ya hesabu za halmashauri hiyo kwa mwaka huo wa fedha, Mkaguzi Mkazi Mkoa wa Kigoma, Exaud Nikutusya alisema kuwa kuchelewa kutekelezwa kwa miradi hiyo kunachelewesha maendeleo ya wananchi.

Akitoa maelezo kuhusiana na jambo hilo alisema kuwa kwa mwaka huo wa fedha halmashauri ilipokea Sh bilioni 4.6 kutoka serikali kuu na wafadhili kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kulikuwa na kiasi cha Sh bilioni 1.6 kilichobaki mwaka uliopita na kufanya halmashauri hiyo kuwa na jumla ya Sh bilioni 6.2 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Hata hivyo alisema kuwa kutokana na fedha hizo, halmashauri iliweza kutumia kiasi cha Sh bilioni 3.7 na kufanya kiasi chaa Sh bilioni 2.7 sawa na asilimia 44 ya fedha hizo kubaki, jambo ambalo alieleza kuwa linawanyima wananchi fursa ya kufaidi miradi hiyo ya maendeleo.

Mkaguzi huyo mkazi alisema kuwa sababu kubwa ambayo inachangia jambo hilo ni kasi ndogo ya Menejimenti ya halmashauri katika utekelezaji wa miradi na hivyo kuchelewesha utoaji huduma kwa jamii.

Akijibu kuhusiana na hoja hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Kigoma, Dominick Kweka alikiri kuchelewa kwa utekelezaji wa baadhi ya miradi na na kusema kuwa Menejimenti inatekeleza miradi ya maendeleo kulingana na fedha zilivyoingia.

No comments: