Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Tuesday, August 23, 2011

52 washikiliwa kwa wizi wa vocha za simu Kigoma


POLISI mkoani Kigoma inawashikilia watu 52 kwa tuhuma mbalimbali zikiwemo za ujambazi wa kutumia silaha na wizi wa vocha za simu za mkononi zenye thamani ya karibu Sh milioni
63.2.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Fraisser Kashai, alisema watuhumiwa 21 wamekamatwa katika Wilaya ya Kigoma Mjini, watuhumiwa 18 wamekamatwa wilayani Kasulu na wengine 13 Kibondo.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa katika operesheni maalumu inayoendelea katika wilaya za mkoa huo ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupambana na vitendo vya kihalifu vikiwemo vya ujambazi wa kutumia silaha, utekaji wa magari na uporaji wa mizigo na fedha za abiria.

Kuhusu na wizi wa vocha za simu, Kamanda Kashai alimtaja mtuhumiwa kuwa ni Itochiman Sebeha (27), mkazi wa Katubuka mjini Kigoma aliyekuwa ni msimamizi na mfanyakazi wa Kampuni ya Shivacom ambao ni wakala wa Kampuni ya simu ya Vodacom.

Alisema kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kunatokana na taarifa zilizokuwa zikikusanywa na makachero wa Polisi mkoani humo waliokuwa wakifuatilia nyendo za mfanyakazi huyo.
Kamanda Kashai alisema baada ya kumtia nguvuni, Polisi waliwasiliana na uongozi wa Shivacom jijini Dar es Salaam ambapo walitumwa wakaguzi wa hesabu mkoani humo na kubaini kuwa fedha za vocha za Sh 63,199,000 zilikuwa hazijapelekwa benki na hazijulikani zilipo.

Alisema wakati wa ufuatiliaji wa nyendo za mtuhumiwa huyo, makachero wa Polisi wakiongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kigoma Mjini, Mohammed Kilonzo, walipata maboksi mawili yaliyojaa vocha za Vodacom yakiwa yamefichwa porini, jambo lililowaongezea shaka katika ufuatiliaji wa nyendo za mtuhumiwa huyo.

Baada ya kuyafanyia ukaguzi maboksi hayo, makachero hao walibaini kuwa yalikuwa na vocha mchanganyiko za Kampuni ya Vodacom zikiwemo za Sh 5,000 kwa kila moja, Sh 2,000, Sh 1,000 na Sh 500.Baada ya kuwasili kwa maofisa wa Kampuni ya Shivacom mkoani Kigoma wakitoka Dar es Salaam, walibaini kuwa maboksi hayo pamoja na vocha hizo, zilikuwa ni sehemu ya zile alizopewa mtuhumiwa huyo kwa ajili ya kuwasambazia wauzaji wa vocha za jumla mkoani Kigoma.

Kamanda huyo alisema Polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na kwamba pamoja na mambo mengine, pia wanashirikiana na wenzao wa Idara ya Uhamiaji ili kubaini uhalali wa uraia wa mtuhumiwa huyo.

No comments: