Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Wednesday, August 24, 2011

Mbaroni kwa kukutwa na SMG, risasi


POLISI mkoani Kigoma, inawashikilia watu wawili raia wa Rwanda na Burundi kwa kukutwa na silaha aina ya SMG na risasi 55 kinyume cha sheria.

Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma, ACP Fraisser Kashai, aliwataja watuhumiwa hao jana kuwa ni Samson Emmanuel (36) raia wa Rwanda na Bizimana Belikimasi (20) raia wa Burundi.

Kwa mujibu wa Kashai, Emmanuel alikutwa na bunduki aina ya SMG katika kijiji cha Busunzu na Belikimasi alikutwa na risasi 55 za bunduki ya aina hiyo akiwa katika kijiji cha Nyagwigima tarafa ya Mabamba wilayani humo.

Kamanda Kashai alisema kuwa watuhumiwa huo walikamatwa juzi usiku kwa wakati tofauti ambapo Belikimasi alikamatwa saa 1.00 usiku na Emmanuel alikamatwa saa 5.30 usiku.

Alisema watuhumiwa wote hao walikamatwa wakiwa katika harakati za kutaka kufanya uhalifu katika maeneo hayo ingawa aliyekamatwa na silaha hakuwa na risasi na aliyekamatwa na risasi hakuwa na silaha.

Kamanda Kashai alisema kuwa bado polisi wanaendelea na upelelezi kama watuhumiwa hao wana uhusiano ama kila mmoja alikuwa na kundi lake la kihalifu.

Alisema kuna uwezekano mkubwa kuwa aliyekamatwa na silaha alikuwa na watu wengine waliobeba risasi na kwa aliyekamatwa na risasi alikuwa na watu wengine waliokuwa na silaha.

Wakati polisi wakiendelea na operesheni na upelelezi wa matukio hayo, pia inawatafuta watu
wengine kutoka katika makundi ya kila mmoja, ili kupata silaha zaidi pamoja na risasi ambazo bado zipo katika mikono hatari ya majambazi kutoka nchi hizo za jirani.

No comments: