Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Tuesday, August 23, 2011

CCM Kigoma wasaka mrithi wa Maranda

 Katibu wa Uchumi na Fedha wa Mkoa wa Kigoma Rajabu Maranda

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Kigoma kimeanza mchakato wa kujaza nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha wa Mkoa iliyokuwa inashikiliwa na Rajabu Maranda ambaye amehukumiwa kwenda jela miaka mitano.

Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Kigoma, Elisha Mwampashi amethibitisha kuanza kwa mchakato huo akisema nafasi hiyo iko wazi baada ya Maranda aliyeshinda katika uchaguzi wa mwaka 2007 kushtakiwa na kufungwa miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia katika kesi ya wizi wa Sh bilioni 1.8 katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Mwampashi amewataja wanachama wa CCM waliochukua fomu na kuzirejesha kuwa ni Nicholaus Zakaria, Yahaya Liheye, Benjamin Charukula na Philipo Misumo ambao baada ya mchujo wataingia katika uchaguzi utakaofanyika kati ya Oktoba mosi na 8, mwaka huu.

Aidha, alisema uteuzi wa mwisho wa majina matatu ya wagombea utafanywa na Kamati Kuu ya CCM Taifa inayotarajiwa kukutana mwishoni mwa mwezi ujao mjini Dodoma.

Mbali ya nafasi ya Maranda, wanaCCM wametakiwa pia kujaza nafasi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi ya CCM mkoani Kigoma baada ya aliyekuwa anashika wadhifa huo, Mussa Chowo kuhamishiwa Dar es Salaam kikazi.

Mwanachama wa CCM wa Tawi la Gungu, Salum Athuman amesema kitendo cha uongozi wa CCM kutotangaza nafasi hiyo ili ijazwe ni makosa kwa kuwa Chowo yuko nje ya Kigoma kwa zaidi ya miaka miwili, hivyo kutokuwepo kwake na pia kutojazwa kwa nafasi hiyo kumechangia kuzorotesha utendaji wa chama.

Mkoa wa Kigoma wenye majimbo manane ya uchaguzi, katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana, CCM iliambulia majimbo matatu huku NCCR- Mageuzi ikitwaa manne na Chadema ikitwaa jimbo moja.

No comments: