Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Monday, August 22, 2011

Zitto aonya mgogoro IPTL kuongeza mgawo umeme

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Zitto Kabwe

MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Zitto Kabwe amesema  kuchelewa kwa mchakato wa kuifilisi Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), kunaweza kusababisha matatizo zaidi ya umeme nchini.
Onyo la Zitto linakuja baada ya mchakato wa kuifilisi IPTL kusimama baada ya Benki ya Standard Chartered kuweka pingamizi Mahakama Kuu kupinga uamuzi uliotolewa awali na Jaji Kaijage, wa kuifilisi kampuni hiyo.

Akizungumzia mchakato huo kwa simu jana, Zitto ambaye tayari kamati yake ilitoa angalizo kwa kutaka kuharakishwa kwa mchakato wa kuifilisi kampuni hiyo, alionya kuhusu mgogoro huo mpya akisema unaweza kusababisha hata uzalishaji umeme kwa IPTL kusuasua na kuingiza nchi katika giza.

Zitto alisema ni wakati sasa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kuingilia kati na kutafuta suluhu ya kudumu kuhakikisha mchakato wa kisheria kuhusu IPTL unamalizika ili kuondoa nchi katika hatari ya kupoteza mabilioni ya shilingi na kuingia kwenye giza.
"Mwanasheria Mkuu au Waziri wa Sheria na Katiba wanapaswa kuhakikisha mchakato huu mrefu wa kisheria unakamilika ili jambo hili la IPTL limalizike. Ni jambo ambalo lisipoangaliwa kwa umakini nchi inaweza kuingia katika hatari ya kupoteza mabilioni ya shilingi lakini pia na kuingia katika mgawo mkubwa zaidi wa umeme, "alisisitiza Zitto.

Mwenyekiti huyo wa POAC, alisema hata wakala wa Vizazi, Ufilisi na Vifo (Rita) ambayo tayari ilianza mchakato wa kutafuta kampuni ya kuifilisi IPTL ambayo hutumia fedha za Serikali takriban Sh3bilioni kila mwezi, sasa hivi imesimama na kila kitu kimekwama kutokana na mvutano huo wa kisheria.

RITA yapigwa stop

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa Rita, Philip Saliboko alisema jana Dar es Salaam kwamba mchakato huo wa kuifilisi IPTL ambao ulikwishaanza hivi sasa umesimamishwa baada ya kupokea amri ya Mahakama iliyotolewa na Jaji Mwakibuta.Saliboko alisema tayari walishaanza mchakato wa kutafuta kampuni ya udalali ambayo ingefanya uchunguzi wa mali na fedha za IPTL katika maeneo mbalimbali nchini huku wananchi wenye pingamizi au madai nao wakipewa nafasi.

"Sasa hivi mchakato wa kuifilisi IPTL umesimama kutokana na amri tuliyopewa na Mahakama Kuu. Tumeambiwa tusubiri kwanza kuna pingamizi la Benki ya Standard Chartered kupinga uamuzi huo wa kuifilisi," alisema saliboko.

Alisema kinachosubiriwa sasa na Rita ni uamuzi wa mahakama kuhusu pingamizi hilo la Standard Chartered ili kuona hatima na namna mchakato huo unavyopaswa kuendelezwa hapo baadaye kwa mujibu wa sheria.Alisema pingamizi la Standard Chartered linataka kwanza, kusikilizwa kwa madai yao ya awali ambayo ni kuhusu deni la mkopo dhidi ya IPTL takriban Dola 100 za Marekani (zaidi ya Sh120 bilioni).

Saliboko alisema kutokana na pingamizi hilo, mchakato huo wa kulisikiliza unatarajiwa kuanza Agosti 24 na kusisitiza kwamba kitakachokuwa kikiendelea ni mchakato wa kisheria hadi uamuzi wa mwisho kuhusu hatima hiyo ya kuifilisi.

Wiki moja iliyopita, Rita ilitoa tangazo katika vyombo vya habari ikisema, “kwa amri ya mahakama iliyotolewa na Mheshimiwa Jaji ( Semstocles) Kaijega, Julai 15  2011 katika Mahakama Kuu ya Tanzania kwenye shauri namba 254, la mwaka 2003 na shauri namba 49 la mwaka 2002, mpokezi rasmi ameteuliwa kuwa mfilisi wa kampuni tajwa (ITPL) bila ya kamati ya uchunguzi.”

Uamuzi wa Mahakama Kuu
Julai 15 mwaka huu, Mahakama Kuu chini ya Jaji  Kaijage, ilitoa uamuzi huo katika kesi ya madai namba 254 ya mwaka 2003 iliyofunguliwa na Kampuni ya Vip Engeneering and Marketing Ltd dhidi ya IPTL, Mechmar Corporation (Malaysia) Berhad na Mfilisi.

Katika hukumu hiyo, Jaji Kaijage alifafanua kwamba kutokana na ombi lililowasilishwa Februari 25, mwaka 2002, na Kampuni ya Vip Engeneering and Marketing ambayo ni mmoja wa washirika wa IPTL na baada ya kupokea maelezo ya mawakili wake kwa njia ya maandishi na ombi hilo kuchapishwa na Gazeti la Serikali Oktoba 10,2003, aliamuru kampuni hiyo ifilisiwe.

1 comment:

Anonymous said...

Kuna watu huenda hawajui kabisa wajibu na nafasi zao katika kufanya maamuzi yenye maslahi na umma ndani ya wakati. Kila kukicha mambo yanharibika ukiuliza eti kuna mtu/watu fulani walizembea kuchukua hatua stahili ndani ya wakati. Hii mpaka lini?