
Sokwe wa Hifadhi ya Taifa ya Gombe
BUNGE limepitisha azimio la kurekebisha mpaka na upanuzi wa
Hifadhi ya Taifa ya Gombe iliyopo mkoani Kigoma ambapo sasa ukubwa wake
utaongezeka kutoka kilometa za mraba 33.74 kufikia 56.
Katika marekebisho ya hifadhi hiyo iliyoanzishwa mwaka 1968
yenye sokwemtu, itahusisha kuondolewa kwenye hifadhi eneo la kilometa za mraba
0.2 lenye makaburi, mashamba na nyumba saba pamoja na kuongezwa ufukwe wenye
kilometa za mraba 1.26.
Pia kuongezwa kwa ukanda wa maji wenye ukubwa wa kilometa za
mraba 21. Katika maamuzi hayo, hakutakuwa na fidia yoyote.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki
alisema marekebisho hayo yataimarisha uhifadhi na ulinzi wa wanyamapori walio
hatarini kutoweka hususan sokwemtu; kuboresha uhifadhi wa bionuwai yakiwamo
mazalia, makuzio, makazi, maficho na malisho ya samaki na viumbe wengine wa
majini.
“Kuongeza shughulil za utalii kama
kuogelea, utalii wa mitumbwi na uvuvi wa burudani na kudhibiti mapato
yaliyokuwa yanapotea kutokana na watalii kuona sokwemtu bure,” alisema Balozi
Kagasheki.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli aliitaka Serikali kuweka alama ya
mpaka wa hifadhi katika eneo la ziwa mara mpaka rasmi utakapojulikana ili
kuepusha migogoro baina ya Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa na wananchi wavuvi.
Akichangia azimio hilo,
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) alisema katika hifadhi hiyo
ya Gombe, watalii wanaotembelea wameongezeka kutoka 700 mwaka 2008 na kufikia
2,600 mwaka jana na kuongeza, “naomba sasa uwanja wa ndege uitwe wa
Gombe-Mahale ili kuvutia watalii kuja Kigoma”.
Mbali na Hifadhi ya Gombe, pia Bunge limepitisha azimio la
kupandishwa hadhi Pori la Akiba la Kisiwa cha
Saanane kilichopo mkoani Mwanza ambapo sasa litatambulika kama
Hifadhi ya Taifa ikijumuishwa na visiwa vya Chankende Kubwa na Chankende Ndogo
na eneo la maji linalozunguka visiwa hivyo.
Kwa mujibu wa Balozi Kagasheki, hifadhi hiyo ina ukubwa wa
kilometa za mraba 2.18 kwa kujumuisha pori
la Saanane lenye kilometa za mraba 0.76, visiwa vya Chankende Kubwa na Ndogo
vyenye kilometa za mraba 0.1 na eneo la maji linalozunguka visiwa lenye ukubwa
wa kilometa za mraba 1.32.
Alisema pori hilo lililoanzishwa mwaka
1964 lilikuwa na lengo la kuhifadhi, kulinda bionuwai na kutoa burudani kwa
wakazi wa Mwanza na mikoa ya jirani.
Pori hilo lina mimea, wanyamapori waishio majini
na nchi kavu na mandhari ya miamba na majabali makubwa.
No comments:
Post a Comment