Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Monday, September 3, 2012

Wakimbizi waombwa kujiorodhesha kurejea nyumbani kwa heshima

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Silima
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Silima


SERIKALI ya Tanzania imewataka wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa katika Kambi ya Mtabila wilayani Kasulu mkoani Kigoma, kutumia vizuri muda uliobaki kuanzia sasa hadi Desemba 31, kujiorodhesha kwa hiari ili kurudishwa nchini kwao kwa heshima.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Silima alisema hayo katika Kambi hiyo ya wakimbizi na kuonya kuwa baada ya muda huo hali itakuwa ngumu kwa wakimbizi hao.

Pia alielezea kutoridhishwa na kasi ndogo ya wakimbizi hao kujiorodhesha kurudishwa nchini kwao kwa hiari tangu wafutiwe hadhi ya ukimbizi na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emanuel Nchimbi Agosti mosi mwaka huu


Alisema hadi kufikia Desemba 31 mwaka huu, wakimbizi wote watarejeshwa kwa hiari na kwa kufuata utaratibu wa Sheria za Kimataifa za kuwarudisha wakimbizi
Kutokana na hilo ametoa mwito kwa wakimbizi hao kuliangalia jambo hilo kwa makini kabla muda haujaisha.

Akisisitiza, Silima alisema baada ya muda huo kupita, hadhi yao itabadilika kwani kwa sasa hawana hadhi ya ukimbizi waliyokuja nayo na ndiyo maana Tume ya Pande Tatu imeona ni jambo la maana kuwarudisha wakimbizi hao nchini kwao Burundi.
Alisema wakimbizi hao wanaonekana kupuuza mwito na agizo la Serikali ya Tanzania lililotolewa kwa niaba ya Tume ya Pande Tatu la kuwataka kurejea nchini mwao.
Silima alisema tangu wakimbizi hao wafutiwe hadhi ya ukimbizi hakuna jitihada zozote wanazoonesha za kuunga mkono suala la kurudi nchini mwao.

Mkuu wa Wilaya Kasulu, Dahn Makanga alisema kusuasua kwa wakimbizi hao kujiandikisha kurudi nchini mwao kwa hiari, kunaonesha hawataki kutumia nafasi hiyo kurudi kwa hiari na kwa heshima kama ambavyo Serikali ya Tanzania, Burundi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) walikubaliana

No comments: