WALIMU mkoani Kigoma wamezituhumu
baadhi ya taasisi za fedha mkoani humo kwa kuwaingiza kwenye mikopo bila ridhaa
zao na kufananisha na utapeli.
Mwenyekiti wa Katibu wa Chama cha
Walimu Mkoa Kigoma, Saidi Ndee alisema yapo malalamiko ya walimu kuwa asasi
hizo zimetafuta hundi namba za walimu bila wahusika kujua na kujikuta wakiwa
kwenye mikopo jambo ambalo wengine hawakuwa tayari kuchukua mikopo hiyo.
Ndee alisema kuwa kitendo hicho ni
sawa na uhuni ambapo ameitaka Serikali kuchukua hatua madhubuti katika
kukomesha vitendo hivyo na kinyume cha maadili ya taasisi za fedha kinachofanywa
na taasisi hizo.
Kulingana na taarifa hizo Katibu wa
CWT Wilaya ya Kasulu, Lucy Masegenya aliwataka walimu wote ambao waliingizwa
kwenye mikopo na taasisi hizo, ikiwemo ya Bayport bila ridhaa yao kuwasilisha
vielelezo vyao ofisini kwake ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Maseganya alisema kwa kiasi kikubwa
taasisi hizo za fedha licha ya kufanya kitendo hicho kinyume na maadili ya
taasisi za fedha, lakini pia zimekuwa zikitoza riba kubwa ambayo imekuwa mzigo
mkubwa kwa walimu na mikopo hiyo kutokuwa na manufaa yoyote.
Sambamba na hilo Katibu huyo alisema
taasisi hizo za fedha zimekuwa zikienda Hazina Ndogo mkoani humo na kuzungumza
na watendaji wa ofisi hiyo, na kufanikisha mkakati wao wa kuwaingiza walimu
kwenye mikopo bila ridhaa yao na kuanza kuwakata marejesho kila mwezi.
Meneja wa Bayport Mkoa Kigoma,
Jackson Kakwaya alikanusha kuwepo kwa vitendo vya taasisi hiyo bila ridhaa yao.
Hata hivyo Meneja huyo amekataa kutoa
maelezo kwa kile alichoeleza kuwa hana mamlaka ya kuisemea taasisi hiyo na
badala yake alitaka jambo hilo aulizwe Mwakilishi Mkazi wa Bayport nchini
aliyefahamika kwa jina la Mica ambaye hata hivyo simu yake haikupatikana.
No comments:
Post a Comment